MAAFISA, ASKARI 14 WA TAWA WAVISHWA VYEO VIPYA VYA JESHI LA UHIFADHI


Maafisa na askari 14 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wamevishwa vyeo vipya baada ya kupandishwa na wengine kubadilishiwa madaraja ya utumishi.


 

Katika hafla hiyo iliyofanyika  Jumamosi, Desemba 18, 2021, katika Makao Makuu ya TAWA, Morogoro, Mgeni rasmi Naibu Kamishna wa Huduma (TAWA), Prosper F. Kyssima, akimwakilisha Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mabula Misungwi Nyanda, amewataka maafisa na askari hao kuvitendea haki vyeo hivyo kwa kutimiza majukumu yao kwa weledi katika maeneo yao ya kazi huku wakizingatia nidhamu ya kijeshi kwa mapana yake.
 

Pia amewaelekeza maafisa na askari wa TAWA kuzingatia nidhamu katika jeshi ikiwa ni pamoja na kuzingatia mahudhurio ya paredi zotezilizowekwa kwa mujibu wa utaratibu.
 

Amesisitiza, wanatakiwa kumheshimu aliyewazidi na waliyemzidi cheo, kuwa nadhifu wa mavazi na mwenendo wa jumla mahali pa kazi na katika jamii.
 

“Ni imani yangu kwamba vyeo mlivyovishwa kijeshi vitawaongezea nidhamu, ujasiri na kujiamini pale mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu,” amesema Kyssima.
 

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi Operesheni, Mlage Kabange, amesema TAWA itaendelea na utekelezaji wa agizo la serikali la kubadili mfumo wa uendeshaji kutoka mtindo wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi, kwa maafisa na askari wake maeneo yote.
 

Amesema katika kuthibitisha azma hiyo, hadi sasa kuna maafisa na askari 150 wanaoendelea na mafunzo katika Chuo cha Likuyu Sekamaganga, ambao wanatarajiwa kuhitimu Desemba 22, mwaka huu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments