CCM YAJIPANGA KUADHIMISHA MIAKA 45 YA CCM...YAPOKEA TAARIFA DOSARI YA MIENENDO YA POLEPOLE, GWAJIMA NA JERRY SLAA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, December 19, 2021

CCM YAJIPANGA KUADHIMISHA MIAKA 45 YA CCM...YAPOKEA TAARIFA DOSARI YA MIENENDO YA POLEPOLE, GWAJIMA NA JERRY SLAA


 Shaka Hamdu Shaka

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog, DODOMA

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imekutana  jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine imepokea na kujadili  kujiweka tayari juu ya maandalizi ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama hicho.

Akizungumza Desemba 18,2021 na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa vikao vya Kitaifa vya chama hicho Katibu Mwenezi wa Chama hicho  Shaka Hamdu Shaka amesema uzinduzi utafanyika Januari 29 katika  mkoa wa kusini wilaya ya kusini Unguja huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Dkt. Ally Mohamed Shein .

“Juma la maadhimisho litaanza kuanzia Januari 23 hadi Februari 4 mwaka 2022 na Februari  5 itakuwa kilele cha maadhimisho ambapo sherehe hizo kitaifa zitafanyika  mkoani Mara na ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi .”

Shaka amesema,Sherehe hizo zitakwenda sambamba na  matembezi ya mshikamano ili kuwaleta wanaCCM pamoja .

Aidha Shaka amesema maadhimisho hayo yatakuwa ni ya aina yake kwa sababu yanakwenda sambamba na mwaka uchaguzi ndani ya chama hicho ambao unapaswa kufanyika mwaka 2022.

“Maadhimisho haya yatakuwa ya aina yake kwa sababu tunaadhimisha kuzaliwa kwa CCM lakini wakati huo mwaka 2022 ni mwaka wa uchaguzi ,kwa hiyo chama chetu kinakwenda kufanya uchaguzi wa ndani ili kupata viongozi ambao hudumu kwa kipindi cha miaka mitano 2022 hadi 2027”amesema na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo Ujumbe wa miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM ni ‘CCM imara shiriki uchaguzi kwa uadilifu’kwa  maana ya wamba chama kipo imara lakini kinapinga mambo yote maovu ambayo yanaweza kuondoa sifa nzuri ya kupata viongozi wenye uwezo.”

Mbali na hayo amesema Kamati hiyo imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Taifa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia utekelezaji Ilani ya Chama hicho.

“Watanzania wote wamekuwa ni mashuhuda ambapo Rais Samia amekuwa akifanya kazi ya utekelezaji wa ilani kwa ustadi na weledi mkubwa,sisi kama chama tunamuunga mkono na tumeona ni vyema tukampongeza na kumtia moyo kwa kazi kubwa na nzuri ,

“Ukiangalia kwenye utekelezaji wa ilani kijamii,kiuchumi na kisisasa Rais anakwenda vizuri kwa sababu malengo yalioyowekwa katika huduma za kijamii  yamekuwa yakipatikana na kuwekewa mipango na kutekelezwa kwa kiwango kikubwa..,

Amesema katika Nyanja ya kiuchumi nchi imepiga hatua kubwa kwa maendeleo endelevu katika uchumi ambao umenyanyuka kwa kiasi kikubwa.

“Tumeona mheshimiwa Rais kuelekea miaka 60 ya uhuru alielezea namna ambavyo nchi yetu imepiga hatua za kiuchumi kutoka mwaka 1961 hadi 2021 jambo ambalo limedhihirisha kwamba Tanzania sasa inakwenda kupiga hatua kubwa kwa maendeleo endelevu katika uchumi ambao umenyanyuka ambao tumekuwa tukiusisitiza na kuuzungumza siku zote “

Aidha Shaka amesema,Kamati Kuu pamoja na mambo mengine pia imepokea taarifa ya mienendo ya viongozi na wanachama wake watatu Jerry Slaa Mbunge wa Ukonga,Josephat Gwajima Mbunge wa Kawe,na Humphrey Polepole mbunge wa kuteuliwa juu ya dosari na mienendo yao  huku akisema,chama kinaendelea kufuata taratibu za kuwaita kwenye vikao ili wajibu tuhuma zinazowakabili.

“Viongozi kwa hiyo kwa viongozi hawa watatu kuna dosari juu ya mienendo yao na chama kinalifanyia kazi na wataitwa muda wote kuanzia sasa baada ya vikao husika kupangwa ili kuwapa haki yao ya kikanuni na kikatiba ya kusikilizwa.”amesema Shaka na kuongeza kuwa

“Nikiri tu kwamba kweli wameitwa na muda utakapofika watajulishwa rasmi baada ya vikao kupangwa kwa mujibu wa katiba ya CCM,kikao cha kamati kilichokutana  kimeshatoa  maelekezo na hatua inayofuata sasa ni kupanga vikao  na kuwajulisha wahusika ili waweze kufika kwenye vikao hivyo.”amefafanua.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages