WAZEE KAHAMA WAKOSOA KAULI ZA HUMPHREY POLEPOLE, WATAKA CCM IMCHUKULIE HATUA ZA KINIDHAMU

Kutoka kushoto, Charles Gishuli, Khamis Mgeja na Mandwa Khalfani wakijadiliana mambo katika kikao chao.
Baadhi ya wazee ambao ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kahama wakiwa katika kikao cha kujadili mstakabali wa Taifa la Tanzania ikiwa ni miaka 60 ya Uhuru.

Khamisi Mgeja katikati akiwa na baadhi ya wazee wenzake mjini Kahama.
**

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog Kahama

BAADHI ya wazee wa Mjini Kahama mkoani Shinyanga ambao pia ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamepinga vikali kauli za kuikosoa Serikali ambazo zimetolewa hivi karibuni na Mbunge mteule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Humphrey Polepole.

Kauli ya wazee hao imetolewa jana mjini Kahama na wazee kutoka maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga ambao walimtembelea Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Khamis Mgeja kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu mstakabali wa nchi wakati ikitimiza miaka 60 ya Uhuru.

Katika majadiliano yao wazee hao wameelezea kusikitishwa na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na mmoja wa wabunge wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Humphrey Polepole ambazo wamedai zinaweza kuwa chanzo cha kuwagawa watanzania.

Mmoja wa wazee hao ambaye aliwahi pia kushika nafasi ya uwenyekiti wa CCM Mkoani Shinyanga na kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali hapa nchini, Charles Gishuli alisema kauli zinazotolewa na Mheshimiwa Polepole zinapaswa kukemewa na Chama haraka.

Gishuli alisema, Polepole anachokifanya hivi sasa inaonesha wazi kama vile si mwanachama wa CCM na ana lengo la kutaka kuupotosha umma wa watanzania uamini kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hana uwezo wa kuongoza nchi.

“Huyu Polepole ameshika nafasi nyingi za uongozi ndani ya Serikali na Chama, lakini bahati mbaya hivi sasa amesahau kwamba ndani ya Chama kuna taratibu za kukosoana pale panapojitokeza jambo lolote lile lisilo la kawaida,”

“Ki utaratibu ndani ya Chama chetu kuna slogani ya jinsi ya kukosoana, na aelewe kuwa kwenye chama hakuna mwenye mamlaka, mamlaka ni ya vikao, na hata alipokuwa msemaji wa Chama, alikuwa akizungumza baada ya kutoka ndani ya chama, si kama anavyofanya hivi sasa,” alieleza Gishuli.

Alisema hata kama kuna makosa yamejitokeza ndani ya Serikali vyema angetumia utaratibu uliopo ndani ya Chama ambapo ametoa mfano pia wa hivi karibuni alipomkosoa Mheshimiwa mwenzie, Nape Nnauye nje ya utaratibu.

Kwa upande wake Khamis Mgeja aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga alisema kitendo kinachofanywa hivi sasa na Mheshimiwa Polepole kimeonesha wazi madhara ya kuteuliwa watu ambao hawajapata mafunzo yoyote ya kiuongozi.

Mgeja alisema yeye binafsi anashindwa kupata uhalisia wa Polepole, kutokana na kutaka kujionesha yeye ndiye mwana CCM halisi, na hata kudiriki kuwaita baadhi ya watanzania kwamba ni wahuni na mbaya zaidi amekuwa akizungumzia kuhusu nchi baada ya Hayati John Magufuli alishindwa kumaliza wahuni ndani ya chama na ndani ya nchi.

“Sasa jambo kama hili siyo la kufumbia macho, jambo hili ni uchochezi, ni upotoshaji lakini pia ni kupandikiza chuki, ukiangalia mwenendo wa Polepole anayoyazungumza hivi sasa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ni kama anataka kuupotosha umma,”

“Pia ana lengo la kutaka kugonganisha Serikali iliyopo hivi sasa madarakani ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ionekane kwamba kuna tofauti kubwa kati ya Serikali iliyopita na Serikali iliyopo hivi sasa, sasa haya mambo yasipokemewa huyu mtu tutampa nafasi kubwa ya kulipotosha Taifa,” alieleza Mgeja.

Aliendelea kueleza kuwa Mheshimiwa Polepole ana lengo la kutaka aonekane yeye ndiye mwanachama safi wa CCM na msema kweli sana ambapo kiuhalisia ndani ya Chama cha Mapinduzi ana historia yoyote kwa vile kabla ya kuteuliwa katika nafasi ya uongozi wa juu ndani ya CCM hakuwahi kuwa hata Katibu Tawi wa CCM.

Mgeja alisema ni vyema hivi sasa Mheshimiwa Polepole akajirudi na pia amekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kiangalie uwezekano wa kumchukulia hatua za kinidhamu kwa vile kauli anazozitoa zinaweza kuharibu mstakabali wa Taifa la Tanzania pasipo sababu za msingi.

Katika hatua nyingine wazee hao wameelezea kushangazwa na kauli ambazo zimekuwa zikitotolewa na baadhi ya Watanzania za kumlaumu Rais aliyepo madarakani hivi sasa kwamba amekuwa akisafiri mara kwa mara tofauti na mtangulizi wake Hayati John Magufuli.

“Ni mambo ya ajabu kudai Rais anasafiri sana, wanaotoa madai haya hawaelewi umuhimu wa mahusiano ya Kimataifa, na kwamba ili nchi iwe na maendeleo ya haraka lazima iwe na mahusiano na mataifa mengine makubwa ikiwemo suala la kutafuta wawekezaji,” alieleza Charles Gishuli.

Kwa upande wake Mgeja alisema wanaolalamikia safari za Rais Samia ni wavivu wa kufikiri, kwa vile nchi ya Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa na kwamba Taifa la Tanzania bado halijasimama vizuri kiuchumi.

“Jamani Tanzania bado hatujasimama kiuchumi, bado tunatakiwa kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi za nje, na Rais Samia hivi sasa kazi hiyo anaifanya vizuri, ndiyo maana hivi sasa watu wengi wanavutika kuja kuwekeza hapa nchini, na hata suala la kukopa, ukitaka kuendelea lazima ukope,” alieleza Mgeja.

Kuhusu miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania wazee hao walisema Taifa linakwenda vizuri na limepiga hatua katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya barabara na hali ya amani na utulivu imeendelea kuimarika kutokana na uongozi bora uliopo na kwamba kutokana na hali hiyo watu wachache wapotoshaji na wapinga maendeleo hawapaswi kupewa nafasi.

Kwa upande wake mzee Said Hamad mkazi wa Mondo, Kahama Shinyanga yeye binafsi ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa jinsi ilivyojikita katika suala la kuboresha elimu na huduma za afya kwa kujenga mashule, zahanati na vituo vya afya bila kuwachangisha wananchi.

“Mimi kuelekea miaka hii 60 ya uhuru nimefurahishwa na kuridhishwa sana na utendaji wa Serikali hii ya awamu ya sita, ndani ya kipindi kifupi imeweza kufanya mambo makubwa upande wa sekta ya elimu na afya, vyumba vya madarasa vimejengwa zaidi ya elfu kumi ndani ya miezi miwili, haijawahi kutokea,” alieleza Hamad.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments