WIZARA YA MAJI NA BODI ZA MAJI YA MABONDE ZASAINI MAKUBALIANO YA KIUTENDAJI KUENDELEZA USTAWI WA MAZINGIRA

Katibu mkuu Wizara ya maji Mhandisi Anthony Sanga

****

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog, DODOMA.


WIZARA ya maji na bodi za maji ya mabonde nchini zimesaini makubaliano ya kiutendaji na kuahidi kuendeleza ustawi wa mazingira kwa kuhamasisha jamii kuheshimu sheria za mazingira hasa kufanya ujenzi ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji.


Hafla hiyo ya makubaliano imefanyika leo jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau wa maji pamoja na Maafisa mabonde ambao wameeleza kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya ukusanyaji na utupaji wa taka zinazozalishwa majumbani Ili kulinda vyanzo hivyo.


Akiongea katika hafla hiyo Katibu mkuu Wizara ya Maji  Mhandisi Anthony Sanga ametoa wito kwa bodi za maji za mabonde kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya Tabia  nchi ikiwemo ukame na uhaba wa maji pindi mvua zinapochelewa kunyesha.


Amesema licha ya  bodi hiyo kuonyesha ufanisi mzuri wa kazi  kutoka asilimia 52.2 Mwaka 2019/2020 hadi asilimia 75 kwa Mwaka 2021  lakini bado wanapaswa kuongeza nguvu  katika maeneo mbalimbali ikiwemo usamizi wa vyanzo vya maji kuvitambia na kuviwekea mipaka  kwakuwa Kasi ya utunzaji wa vyanzo hivyo sio nzuri  vimekuwa vikivamiwa.


"Bodi zote nchini zinapaswa  kuhakikisha zinajenga Tabia ya kukagua vibali vya maji wanavyotoa kwa watumiaji wa maji katika maeneo yao ili kuhakikisha watu wanaotumia maji hayo  wakiwemo wakulima na wafugaji wanatumia kulingana na vibali vinavyowaelekeza,


"Jengeni tabia ya kukagua vibali mnavyowapatia watumiaji wa maji katika maeneo yenu ya kazi,wakulima wanafanya kilimo cha umwagiliaji, wafugaji wanaotumia maji kwa ajili ya kunywesha mifugo yao pamoja na watumiaji wa majumbani muwakague vibali vyao ili waweze kufahamu wanatakiwa kutumia maji kiasi gani na kwa muda gani kulingana  na vibali mlivyowapa,"amesisitiza.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewaomba Maafisa maji hao wa mabonde ya maji kutekeleza wajibu wao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufuata  maelekezo ya viongozi  wa juu na  kutokusubiri hadi viongozi hao kuchukua hatua.


"Niwaombe sana tuwasaidie viongozi wetu ,nyinyi ni mabalozi twende tukawasaidie viongozi wetu kwa kufanya kazi kwa kujituma ,maji ndiyo kila kitu kumekuwa na tabia ya kusubiri hadi viongozi wa ngazi ya juu kufika katika maeneo yetu ya kazi kutatua changamoto ambazo hata nyie mnaweza kuzitatua tabia hiyo muache ",amesema.


Kwa upande wake Afisa Maji wa bonde la Ruvu Wami Elibariki Mmasi amesema   mkataba huo utawapa njia ya kuhakikisha wanajitathmini kazi walizozifanya kwa kipindi cha mwaka mzima na kwamba  kutokana na mabadiliko ya Tabia ya nchi  hasa Mwaka huu ambapo mvua zimechelewa kunyesha  wao wamejipanga kuhakikisha hakuna tabu yoyote ya maji.


Aidha ametoa  rai  kwa jamii kutumia maji kwa uangalifu mkubwa ili kuyalinda kwa vizazi vyote huku akiahidi kwa niaba  ya Maafisa wengine wa bodi hiyo  kuwa watahakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa nguvu zote.


"Kwetu sisi  tunatambua kuwa lengo la wizara na serikali ni kuwezesha vizazi vya sasa na vya baadae kutumia maji yaliyopo,tunatambua dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuhakikisha maji yanapatikana hivyo tuwahakikishie wadau wote kuwa Maji watapata maji ya uhakika  kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa", amesema.


Ameendelea kusisitiza kuwa ustawi wa mazingira una haribika kwa mfano katika maeneo ya bahari kuna ustawi mkubwa sana wa mikoko ambayo ni hazina ya Taifa ambayo hutakiwi kuikata kwa sheria ya misitu kwa maana hiyo katika maeneo kama hayo hutakiwi kujenga wala kuendeleza kitu chochote.


Mikataba hiyo ya makubaliano ya utendaji kazi kati ya wizara na Bodi za maji za mabonde husainiwa kila Mwaka kwa lengo la kupima utendaji kazi wa bodi za maji za mabonde ambapo kwa mwaka huu umehusisha  mabonde 9 ikiwemo Wami-Ruvu, Rufiji, Ziwa Victoria, Tanganyika, ziwa Nyasa,Pangani ,Rukwa, Ruvuma na Pwani ya Kusini pamoja na bonde la Kati

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments