WADAU WA HAKI ZA BINADAMU WATAKA VIJANA AMANI ,HAKI NA WAJIBU KWA JAMII

Afisa habari wa kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNIC) Stella Vuzo .

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Dkt. Fatma Rashed Khalfan

***


Na Dotto Kwilasa Malunde 1 Blog, DODOMA.

KUELEKEA siku ya kimataifa ya Maadhimisho ya haki za binadamu Desemba 10 ,Umoja wa mataifa (UN) kwa kushirikiana na Tume ya haki za binadamu na utawala Bora nchini (THBUB) wamewataka Vijana nchini hapa kuwa mstari wa mbele na kusimama kidete kutetea haki za binadamu kwa kuzingatia  malengo ya maendeleo endelevu ambayo ndani yake kuna lengo  la 16 linaloangazia kuwepo kwa amani,Taasisi madhubuti na haki Kwa jamii.


Hayo yamejiri  Jijini Dodoma wakati wa mdahalo wa wazi kati ya wadau wa masuala ya haki za binadamu na wanafunzi wa kada ya Sheria katika chuo kikuu Cha Dodoma (UDOM) uliolenga kuchochea uelewa wa utii wa haki kwenye makundi maalumu na mengineyo.

Akiongea katika mdahalo huo ,Afisa habari wa kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNIC) Stella Vuzo  amesema  kwa mwaka huu wameamua kuanzimisha siku hiyo kupitia mdahalo wa wazi kwa kuwashirikisha wanafunzi wa sekta ya Sheria katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Ili kuwaandaa kutumika kutetea haki Kwa watu wanaoikosa.


Aidha amesema wao kama wadau wa haki hizo wameangazia kauli mbiu ya mwaka huu ambao ni kupunguza tofauti ili kuleta haki za binadamu wanahakikisha kwamba wanafunzi hao  wanakuwa na uelewa wa haki na wajibu katika jamii .


"Kuna suala zima la haki za binadamu linalopaswa kuazingatiwa na kutiliwa mkazo kwenye jamii yetu,kwa utofauti uliopo wa makundi unachekewesha watu wengine kupata haki zao za msingi,Vijana wanapaswa kuelewesha jamii kwamba haki ni wajibu na msingi wa Maendeleo,"ameeleza Afisa huyo wa Umoja wa mataifa .


Ameeleza kuwa kupitia mdahalo huo ,wamewaelimisha wanasheria hao Vijana  kuhusiana na kufuata misingi ya  malengo ya maendeleo endelevu ambayo ndani yake kuna lengo  la 16 linaloangazia kuwepo kwa amani,Taasisi madhubuti na haki.


"Kuna lengo la 10 pia linalozungumzia kuwepo kwa kupunguza tofauti za kijamii ili kupatikana haki kwa watu wote,katika hili tunawahamasisha vijana waweze kujitambua na kuyaenzi malengo malengo hayo  na kuyaishi ili kukabiliana na changamoto za dunia,"amefafanua.


Vuzo amebainisha kwamba Siku ya haki za binadamu ni kilele cha siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na wasichana hivyo vijana  wanapaswa kutambua wao ni sehemu ya kutatua hilo tatizo kwa vitendo bila kusubiri kusukumwa.


"Kwa kuwa wao wanasomea Sheria sisi tunawachukulia kama watetezi na wasimamizi wa haki za binadamu,tunaamini wanaweza kusaidia watu kwa kuwapa msaada wa kisheria na kuwashauri watu ambao wameathirika na masuala ya kijinsia ili wawe salama,"amesema.


"Kikubwa zaidi tumekuwa na mwendelezo mkubwa wa jinsi ya kuwashauri vijana na jamii kwa ujumla masuala yote ya haki za binadamu na kulenga  kupunguza utofauti,tumewaelimisha wanafunzi hawa kwa kuamini kuwa watakuwa manalozi wazuri,"amesema.

Kwa upande wake Kamishna wa tume ya haki za binadamu na utawala Bora (THBUB) Dkt.Fatma Rashed Khalfan ametumia nafasi hiyo kueleza ujumbe wa tume hiyo ikiwa ni siku ya haki za binadamu na kusema kwamba wao kwa kuungana na wadau wa Umoja wa mataifa na wanafunzi wa sheria UDOM wataendeleza  kuhamasiaha misingi ya utawala Bora na kuheshimi utu wa mtu katika jamii.


Dkt. Fatma ameeleza mapendekezo ya tume hiyo kuwa ni muhimu kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali zote mbili kuhusu haki za binadamu kwa kuzingatia Sheria ,sera na mikakati mbalimbali inayofanywa katika kulinda haki.


Amefafanua kuwa wao kama tume inayosimamia utu na haki wamekuwa wakishirikiana na wadau mbali mbali kuangalia hoja zinazoibuliwa kuhusu masuala ya haki za msingi za kibinadamu ili kupata muelekeo wa pamoja na kuenzi haki kupitia wajibu.


"Ni muhimu kutambua jitihada kubwa zimefanyika kuhusu watu wenye ulemavu na kwa wanafunzi wa kike, tunashuhudia Serikali ikiwa inafanya marekebisho ya kanuni zinazombana mwanamke,"amesema.


Hata hivyo Kamishna huyo wa THBUB ameeleza kuwa pendekezo lao  kubwa bado ni  kuangalia sera ,Sheria na mikakati ya kuhakikisha kunakuwepo  mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kike walioruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua wanakuwa salama.


"Tunatambua kwenye jamii bado kuna unyanyasaji wa kijinsia kuhusu Watoto wa kike,suala hili tunalisimamia zaidi ili kumlinda mtoto wa kike abaki salama na kuwa na mazingira mazuri ya kupata elimu bila kubugudhiwa,na hii ndiyo maana halisi ya haki za binadamu,"amesema.


Pamoja na mambo mengine,kiini cha maadhimisho ya Siku ya haki za binadamu ni kuelimisha na kuhamasisha watu kulingana na binadamu alivyo na kukumbusha hatua zilizopigwa na jamii katika kutekeleza sula la heshima ya binadamu wote, dhidi ya utumwa na kukandamizwa kwa haki binafsi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments