WAHAMIAJI HARAMU 33 NA WATANZANIA SITA WAKAMATWA KAHAMA

Basi aina ya TATA linalojulikana kwa jina la SUDENS lenye usajiri wa namba T 478 DEH linalofanya safari zake kati ya Kahama na Tabora likiwa limeshikiriliwa na Idara ya Uhamiaji wilaya ya Kahama baada ya kukamatwa katika mji mdogo wa Kagongwa , Manispaa ya Kahama likiwa limebeba Wahamiaji haramu 9 raia wa nchi za Rwanda na Burundi likiwasafirisha toka mjini Kahama. Picha na Patrick Mabula.
Basi aina ya TATA linalojulikana kwa jina la SUDENS lenye usajiri wa namba T 478 DEH linalofanya safari zake kati ya Kahama na Tabora likiwa limeshikiriliwa na Idara ya Uhamiaji wilaya ya Kahama baada ya kukamatwa katika mji mdogo wa Kagongwa , Manispaa ya Kahama likiwa limebeba Wahamiaji haramu 9 raia wa nchi za Rwanda na Burundi likiwasafirisha kutoka mjini Kahama
Afisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kahama Salum Rashid Salum akionesha wahamiaji haramu wapatao 19 wakiwa kwenye gari la idara hiyo baada ya kuwakamata juzi mjini Kahama katika stendi ndogo ya CDT mjini hapa. Picha na Patrick Mabula.

&&&&


Na Patrick Mabula , Kahama.

Idara ya Uhamiaji wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga imewakamata wahamiaji haramu 33 kutoka nchi za Rwanda na Burundi pamoja na Watanzania sita (6) wanaotuhumiwa kujihusisha kuwasafirisha kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Uhamiaji wa mkoa wa Shinyanga ,Rashid Mageta amesema wahamiaji haramu hao walikamatwa kwa nyakati mbalimbali katika meneo ya Manispaa ya Kahama wakiwa wameingia nchini kinyume cha sheria na taratibu za uhamiaji.

Mageta amesema Idara ya Uhamiaji imewakamata wahamiaji hao pamoja na baadhi ya Watanzania wanaotuhumiwa kuwasafirisha na magari yao na tayari hatua mbalimbali za kisheria zimechukuliwa ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Akifafanua walivyokamatwa amesema kati ya wahamiaji hao 9 walikamatwa katika mji mdogo wa Kagongwa wakiwa kwenye basi la SUDENS aina ya TATA lenye namba T 478 DEH mali ya kampuni ya Salum Transport wakiwa wakisafirishwa kutoka mjini Kahama kupitia Tabora kwa madai walikuwa wanaelekea nchi za Namibia na Msumbiji.

Mageta amesema kati ya wahamiaji hao 33 waliofikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika ni 14 na wapatao 8 wameshahukumiwa kulipa faini ya shilingi 500,000 au kifungo cha miezi mitatu jela na hakuna aliyelipa faini wote walikwenda kutumikia kifungo hicho.

Amesema kwa upande wa idadi ya wahamiaji 19 waliobaki kesi zao zinaendelea kwenye mahakama ya wilaya ya Kahama pamoja na Watanzania wanaotuhumiwa kujihusisha kuwasafirisha watu hao kwa kutumia magari yao ya abiria ambayo nayo yanashikiliwa na Uhamiaji.

Magesa amewataja Watanzania waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kuwasafirisha raia wa kigeni kuwa ni Lednard Daniel (32) dereva wa basi la SUDENS , kondakta wake Mbongo Said (52) pamoja na mawakala wa gari hilo Mwesigwa Ramadhan (42) na Naomi Peter (28) ambao wapo mahabusu baada ya kushindwa masharti ya dhamana ya shilingi Milioni10 na nyumba yenye thamani hiyo hiyo.


Amesema Watanzania wengine waliofikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kahama kwa tuhuma ya kusafirisha wahamiaji hao kwa gari yao ni dereva wa HIACE inayoitwa Vatican City (Mungu Mkubwa) yenye namba T 608 DWN , Mtalemwa Kashumba (42) na kondakta wake Juma Samwel (25) waliodaiwa kuwabeba kutoka Runzewe wilayani Bukombe hadi stendi ndogo ya CDT mjini Kahama.

Kwa upande wake Afisa uhamiaji wa wilaya ya Kahama Salum Rashid Salum akiongea kwa niaba ya Mageta amesema wamebaini kuwepo kwa mtandao wa watu wanaotuhumiwa kujihusisha na usafirishaji wa raia wa kigeni na kuja hapa nchini na tayari wameanza kufanyia kazi swala hilo ili kuhakikisha wanaohusika wanakamatwa na sheria inachukua mkondo wake.

Salum amesema wilaya ya Kahama kwa kipindi hiki kifupi inakabiliwa na wimbi kubwa la wahamiaji haramu kuingia hasa katika Manispaa ya Kahama na kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kukabiriana na tatizo hilo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa.

Aidha idara ya uhamiaji mkoa wa Shinyanga imetoa wito kwa wananchi na raia wema kushirikiana na idara hiyo na kuwataka wenye magari ya kubeba abiria wanaojihusisha kusafirisha raia wa kigeni kuacha mara moja na atakayebainika atachukuliwa sheria kali , kutozwa faini kuanzia shilingi milioni tano, kifungo pamoja na kutaifishwa gari lake kwa mujibu wa sheria ya uhamiaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments