Breaking

Post Top Ad

Friday, November 19, 2021

VIJANA 71 SHINYANGA WAHITIMU MAFUNZO YA UANANGENZI, WAISHUKURU SERIKALI KWA KUWAPATIA FURSA YA KUJIAJIRIMeneja wa Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) mkoani Shinyanga, Hopeness Elia (kushoto) akitoa taarifa mbele ya mgeni rasmi , Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi katika Hafla ya wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi yaliyotolewa na Shirika la SIDO.
**

JUMLA ya Vijana wapatao 71 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Shinyanga wamehitimu rasmi mafunzo ya Uanangezi ambayo yametolewa na Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo vidogo nchini (SIDO) mkoani Shinyanga.

Mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia vijana hao kuweza kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira kutoka Serikalini ama katika Taasisi za Umma na pia kuweza kuendesha familia zao bila ya kuwa tegemezi.

Mafunzo hayo ni pamoja na usindikaji wa vyakula, uchomeleaji, ushonaji, ufundi wa magari, utengenezaji wa viatu na usindikaji wa ngozi.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Meneja wa SIDO mkoani Shinyanga Hopness Kweka mbela ya mgeni rasmi, Katibu Tawala ya wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi ambaye amemwakilisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko mafunzo hayo yametolewa kwa siku 16.

“Mheshimiwa mgeni rasmi mradi huu umechukua siku 16 ambao umeanza Novemba 4, mwaka huu na unahitimishwa leo Novemba 19, 2021, kiuhalisia kwa mradi wa kupeleka wanangenzi kujifunza ujuzi kwa ajili ya kujiajiri na kuajiri wengine bado muda huu ni mfupi ila kutokana na uwezo wa fedha na muda tuliopewa ilibidi tujibane katika muda huo,”

“Mheshimiwa mgeni rasmi mbele yako kuna vijana 71, miongoni mwao wanawake 25 na wanaume ni 46 na umri wao hauzidi miaka 35 wote wako chini ya hapo mpaka miaka 18, vijana hawa tunategemea baada ya kupata mafunzo haya na ujuzi huu, wataenda kujiajiri wenyewe na kutengeneza ajira kwa watu wengine,” ameeleza Kweka.

Kweka ameendelea kufafanua kuwa ni rai ya SIDO kuona lengo la mradi kama lilivyoandikwa kwamba ni kuwapa elimu na ujuzi ili wakatengeneze ajira kwao na kuajiri vijana wengine ikiwa lengo la msingi ni kutengeneza vipato kwao, vipato vya familia zao na kuchangia uchumi wa Taifa.

Amesema pamoja na vijana hao kuhitimu mafunzo yao bado Shirika la SIDO kama Taasisi ya Serikali litakuwa bega kwa bega na vijana hao katika kuhakikisha hawarudi nyuma kwa vile ni vijana ambao wametoka katika wilaya zilizopo katika mkoa wa Shinyanga.

Katika risala yao kwa mgeni rasmi wahitimu hao wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo kwa namna moja ama nyingine yatawasaidia kuweza kujiajiri wenyewe hali itakayowawezesha kuendesha vyema familia zao na kujiongezea kipato.

“Ndugu mgeni rasmi katika mafunzo haya tumejifunza kwa vitendo fani mbalimbali mfano uokaji wa mikate, maandazi, skonzi, keki na kadhalika, uchomeliaji, ufundi magari, ushonaji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi,”

“Ndugu mgeni rasmi elimu na mafunzo tuliyopatiwa itatusaidia kuboresha uendeshaji wa kazi na uzalishaji bidhaa kwa tija ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya mkoa na nje, na tunaushukuru uongozi wa SIDO na wizara ya elimu na ufundi kwa kutoa mafunzo haya ambayo yameamsha ari ndani yetu ya kujiajiri wenyewe,” imeeleza sehemu ya risala.

Pia wahitimu hao wamesema pamoja na kuhitimu mafunzo ambayo wamepatiwa bado wana changamoto kadhaa zinazowakabili ikiwemo upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuendeshea shughuli zao watakazozianzisha.

Katika hotuba yake mgeni rasmi, Boniface Chambi amewapongeza wahitimu hao kwa kuitikia wito wa Serikali unaowataka vijana kutumia fursa zilizopo hapa nchini na kuweza kujiajiri wao wenyewe.

Chambi amesema kutokana na mafunzo ambayo wamepatiwa wataondokana na changamoto ya kuhangaika kutafuta ajira za maofisini ambapo amewataka wajipongeze wao wenyewe kwa kupata fursa hiyo miongoni mwa vijana wengi walioko mkoani Shinyanga.

Kuhusu changamoto ya ukosefu wa mitaji, Chambi amewashauri vijana hao kuunda vikundi miongoni mwao kulingana na fani walizojifunza na waweze kuomba mikopo kutoka katika Halmashauri zao ambako kuna mfuko wa kuwakopesha vijana, wanawake na walemavu.

“Nendeni mkafanyie kazi ujuzi huu mlioupata, pamoja na kwamba mmetoa changamoto ya mitaji, niwaombe baada ya hapa nendeni mkaunde vikundi vyenu vya watu watano watano, kisha pelekeni maombi katika Halmashauri zenu, huko kuna mfuko umetengwa kwa ajili yenu,”

“Inawezekana hamfahamu mtapataje mikopo hii, nendeni kwenye kata zenu mtakutana na maofisa Maendeleo ya Jamii, waambieni tayari mna ujuzi na hamna uwezo wa kupata mtaji, na moja ya maelekezo ni kujiunga kwenye kikundi, na kisha mtapeleka maombi yenu Halmashauri mtapatiwa mkopo usiokuwa na riba,” ameeleza Chambi.

Amesema Serikali baada ya kubaini uwepo wa changamoto ya ukosefu miongoni mwa vijana wengi hapa nchini iliamua kuanzishwa kwa mfuko maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Hata hivyo amewaomba wawe makini pindi watakapoanza uzalishaji wa mali zao katika utafutaji wa masoko na kwamba waitumie vyema elimu ya utafutaji masoko ambayo wamepatiwa katika mafunzo yao na moja ya mbinu ni kuhakikisha muda wote wanakuwa na nyuso zinazotabasamu mbele ya wateja badala ya kumnununia mteja.

Hafla hiyo imehitimishwa kwa mgeni rasmi kuwakabidhi rasmi wahitimu vyeti vyao vya kuhitimu ambapo hata hivyo baadhi yao wameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza siku za mafunzo zaidi ili waweze kupata ujuzi wa kutosha.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia mafunzo haya, lakini hata hivyo tunafikiri iangalie uwezekano wa kuongeza siku ili washiriki waweze kupata ujuzi zaidi kutokana na fani tunazofundishwa, maana mfano kwa mafundi makenika, siku 16 hazitoshi, kuna mambo mengi tunakuwa hatujayaelewa, ni vyema wakaongeza siku iwe hata miezi mitatu,” anaeleza Yussuf Mohamedi.
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi akizungumza katika Hafla ya wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi yaliyotolewa na Shirika la SIDO.
Mhitimu wa mafunzo ya Uanagenzi, Janeth Titus akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi.
Wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi wakiwa katika Hafla ya kuhitimu mafunzo ya Siku 16 ambayo yametolewa na Shirika la SIDO.
Wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi wakiwa katika Hafla ya kuhitimu mafunzo ya Siku 16 ambayo yametolewa na Shirika la SIDO.
Wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi wakiwa katika Hafla ya kuhitimu mafunzo ya Siku 16 ambayo yametolewa na Shirika la SIDO.
Wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi wakiwa katika Hafla ya kuhitimu mafunzo ya Siku 16 ambayo yametolewa na Shirika la SIDO.
Wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi wakiwa katika Hafla ya kuhitimu mafunzo ya Siku 16 ambayo yametolewa na Shirika la SIDO.


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages