Na Malaki Philipo na Marco Maduhu Shinyanga
CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoani Shinyanga, kimefanya mahafali ya 36 chuoni hapo, kwa kuwaaga wahitimu wa mwaka wa pili kutoka fani mbalimbali.
Mahafali hayo yamefanyika chuoni hapo leo Ijumaa Novemba 19,2021, na kuhudhuriwa na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na za kifedha, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura.
Akizungumza kwenye Mahafali hayo Kaimu Mkuu wa chuo cha VETA Shinyanga Magu Mabelele, amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1989, ambapo kilikuwa na fani moja ya ujenzi, lakini mpaka sasa kina Fani 37, mafunzo ya muda mrefu yana fani 10 ya muda mfupi fani 27.
Amesema chuo hicho kina watumishi 42, walimu wa mafunzo 28, na 14 wapo katika shughuli zingine saidizi, huku kikiwa na wanafunzi 416 wa Fani ndefu, na 1,364 Fani fupi, na kubainisha kuwawanakabiliwa na uhaba wa Hosteli za wanafunzi, ambapo katika Hosteli za chuoni hapo wana uwezo wa kubeba wanafunzi 170 tu.
“Mgeni Rasmi chuo chetu kwa sasa ni kikubwa sana, ila tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa Hosteli, ambapo wanafunzi wengi wamepanga vyumba mitaani, na hivyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali hasa wa kike na kusababisha baadhi yao kushindwa kumaliza mafunzo,”alisema Mabelele.
“Mfano mzuri wanafunzi ambao wamehitimu leo, walianza mafunzo wakiwa 162, lakini wanahitimu 141, na hiyo inatokana na sababu za kuishi kwenye nyumba za kupanga mitaani (Magheto), ambapo wanakosa uangalizi na kujiamulia mambo yao wenyewe, hivyo natumia fursa hii kuita wawekezaji waje Shinyanga kuwekeza Hosteli za wanafunzi,”aliongeza.
Pia, alisema changamoto nyingine ambayo inawakabili chuoni hapo, ni ukosefu wa huduma ya afya, mfumo wa majitaka ambapo huingia gharama ya kuvuta majitaka kila wiki na hutozwa kiasi cha Sh. 120,000, na kuomba wapunguziwe gharama hizo ili wasiingie hasara, pamoja na kumuomba Mkurugenzi huyo aanzishe usafiri wa umma katika barabara ya Kizumbi, ili wanafunzi wasipate shida ya usafiri.
Katika hatua nyingine alitoa wito kwa wazazi, kuwasaidia watoto wao ambao wanahitimu mafunzo mbalimbali ya ufundi chuoni hapo kwa kuwanunulia vifaa au kuwapatia fedha za mitaji ili wajiajiri wenyewe, kuliko kuwaacha wakilandalanda mitaani na kulalamika hakuna ajira na wakati wanaujuzi wa kutosha.
Aidha Mwanafunzi Elizabeth Philemon akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, alisema changamoto kubwa ambayo inawakabili wahitimu wa mafunzo ya ufundi ni ukosefu wa ajira pale na fedha za mitaji ili wapate kujiajiri wenyewe na ndiyo maana wengi wao huishia mitaani na kukaa bila kazi.
Alisema anaiomba Serikali kupitia Halmashauri zirahisishe masharti ya utoaji mikopo kwa vijana asilimia 4 ili wahitimu hao kutoka VETA wawe wanajiunga kwenye vikundi na kupewa fedha hizo, ambazo zitawasaidia kujiajiri wenyewe na kuacha kutegemea kuajiriwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura, aliwatoa wasiwasi wahitimu wa VETA hasa wale ambao wanaishi Manispaa ya Shinyanga ,kuwa hakuna ugumu wowote wa kupata mikopo tena wao wanafursa kubwa sababu wakipata fedha hizo watakwenda kuzitumia vizuri sababu wana ujuzi na hatimaye kujikwamua kimaisha.
Satura alitoa ahadi pia kwa wahitimu wa fani ya ushonaji na ubunifu wa mavazi kuwa ataangalia namna ya kuwasaidia kwa kuwafungulia ofisi yao ili washone nguo na kujiajiri wenyewe, huku akitoa ahadi kwa wale wa fani za umeme na ujenzi, kuwa watapewa kazi kwenye miradi mbalimbali ya manispaa hiyo ikiwamo ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati,Sekondari ya wasichana, na jengo la ghorofa la utawala la Manispaa.
Akizungumzia suala la usafiri wa umma, alisema Manispaa hiyo hadi kufikia Desemba mwaka huu, wanatarajia kukopesha wafanyabishara magari manne aina ya Coaster, ambayo moja ya masharti ni kubeba wanafunzi, ambapo zitakuwa zikipita katika Barabara za Olshinyanga, Kolandoto, Mwawaza, na Kizumbi.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA.
Social Plugin