ASKOFU SANGU AONGOZA MISA TAKATIFU YA KUFUNGA MWAKA WA KANISA...AWAASA VIJANA KUTOKUBALI KUTUMIWA KUVURUGA AMANI YA NCHI


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akitoa sakramenti ya ubatizo leo katika kanisa kuu la mama mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Jimbo la Shinyanga.


Na Samir Salum - Shinyanga

Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ameendelea kuwasisitiza vijana kutokubali kutumiwa kuvuruga amani ya nchi na badala yake watumie nguvu walizonazo kuujenga  Ufalme wa Mungu.


Askofu Sangu ametoa rai hiyo leo wakati akiongoza Misa takatifu ya kufunga mwaka wa kanisa iliyofanyika katika kanisa kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga ambayo imekwenda pamoja na kufunga kongamano la kijimbo la Vijana Wakatoliki wafanyakazi VIWAWA.


Amesema mara nyingi vijana wamekuwa wakitumiwa kufanikisha mipango ambayo imekuwa ikihatarisha hali ya amani katika mataifa mbalimbali jambo ambalo wanapaswa kulikataa na badala yake watumie nguvu na karama walizonazo katika kuujenga ufalme wa Mungu.


“Mara nyingi vijana wanatumiwa vibaya na watu ambao hawana nia njema kwa sababu wana nguvu sasa wanaweza kutumia nguvu zao vibaya,niwasihi vijana tumieni nguvu zenu katika kujenga ufalme wa mungu kwa kuwa chimbuko la haki,amani,upendo na umoja mahali kote duniani” ,amesema Askofu Sangu.


Askofu Sangu amewataka Watanzania kutochoka kumwomba Mungu ili aendelee kuimarisha misingi ya haki,amani,upendo na mshikamano hatua ambayo itasaidia kuliepusha taifa na  hali ya migogoro na umwagaji damu ambao unatokea katika mataifa mengine kwa sababu tu ya ubinafsi wa watu wachache.


Kwa upande mwingine Askofu Sangu amewapongeza Wanawake Wakatoliki Tanzania WAWATA jimbo la Shinyanga kwa namna ambavyo wamejitoa katika kulilea shirika jipya la watawa la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma ambalo limeanzishwa miaka michache iliyopita.


Amesema WAWATA wamefanya kazi kubwa katika kulilea na kulitunza shirika hilo hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizopo.


“Nichukue Nafasi hii kuwashukuru sana WAWATA wamekuwa mstari wa mbele sana katika mwaka wote huu na miaka iliyopita katika kulitiunza na kulilea shirika letu la Bikira Maria Mama wa Huruma”, amesema Askofu Sangu.


Wakati huo huo askofu Sangu amewaongoza waamini kusali  kuliombea taifa ili lipate mvua za kutosha kutokana na hali ya hewa kwa mwaka huu kutokuwa ya kuridhisha ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alioutoa kwa viongozi wa dini hivi karibuni jijini Mwanza.


Kupitia misa ya leo ambapo pia kanisa linaadhimisha Jumapili ya Kristo Mfalme, Askofu Sangu pamoja na mambo mengine amewabatiza watoto wadogo wapatao 88.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akitoa sakramenti ya ubatizo leo katika kanisa kuu la mama mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Jimbo la Shinyanga.
Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu katika Picha ya pamoja na baadhi ya Vijana walioshiriki kongamano la Vijana wakatoliki wafanyakazi VIWAWA.
Baadhi ya waamini wakiwa katika ibada ya misa takatifu ya kufunga mwaka wa kanisa iliyofanyika leo katika kanisa la Kuu la mama mwenye huruma Parokia ya Ngokolo Jimbo katoliki Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments