VIONGOZI WA TAKUKURU MIKOA 28 WAKUTANA KUTATHMINI UTENDAJI KAZI ...TAKUKURU YAAGIZWA KUWEKA MASANDUKU YA MAONI KUHUSU VIASHIRIA VYA RUSHWA OFISI ZOTE

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa 
akiongea wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU nchini Salum Hamduni akiongea na viongozi mbalimbali wa Taasisi hiyo kwenye mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Jijini Dodoma.
Viongozi wa TAKUKURU kutoka mikoa 28 nchini wakiwa kwenye mkutano huo

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog -Dodoma.

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa nchini(TAKUKURU) kuhakikisha inaweka masanduku ya maoni kuhusu viashiria vya rushwa katika taasisi zote za serikali pamoja na wizara ili kuweza kupokea maoni ya wananchi juu ya viashiria vya rushwa katika taasisi hizo.

Mhe. Mchengerwa ametoa maagizo hay o Novemba 25,2021 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU ambao unatoa fursa kwa viongozi wa TAKUKURU kutathimni utendaji wa kazi wa mwaka mzima uliopita kwa mujibu wa sharia ya kuzuia na kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Waziri Mchengerwa amesema viongozi walio wengi hawatambui kuwa nchi ni ya wananchi hivyo TAKUKURU ina nguvu kubwa katika kupambana na viongozi wasio waaminifu.

"Ndugu zangu maono na fikra zenu zifanye kazi kwa kugusa mioyo ya wananchi wa kawaida katika kupigania vita dhidi ya maadui wa haki, maadui wa haki ambao wamegawanyika katika sehemu kuu tatu, Ujinga, Maradhi na Umasikini,"amesisitiza.

Vilevile ,Mchengerwa amewaagiza viongozi hao kufatilia vyema utekelezaji wa miradi yote ya kimaendeleo inayoendelea hapa nchini na wahakikishe kuwa kusiwepo na mianya ya rushwa.

“Utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo umegubikwa na udanganyifu ninyi kama TAKUKURU kiongozi wa kila wilaya apimwe namna anavyoweza kusimamia matumizi ya fedha katika kila Wilaya na niseme tu kwamba hili ni jukumu letu sote katika kusimamia,

“Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alivyofungua hizi fursa za uchumi hakumaanisha watu watumie fedha hizo vibaya na kutumia nyaraka za uongo kuhusu gharama zinazotumika katika miradi hiyo tumieni mkutano huu kujadili malengo na muhakikishe kusiwepo na mianya ya uchepushaji wa fedha hizo kwaajili ya matumizi binafsi katika kila mradi”,amesema Mchengerwa.


Mbali na hayo ametumia nafasi hiyo kumtaka Mtendaji mkuu wa TAKUKURU nchini Salumu Hamduni,kuhakikisha anatumia nafasi yake kuudhihirishia ulimwengu na watanzania wote kuwa anastahili majukumu haya kwa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa pasipo kumuonea wala kumpendelea mtu yeyote, kuboresha taswira na kuimarisha mifumo ya utendaji kazi za taasisi huku ukilinda maslahi ya Taifa.

" Mheshima Rais anaamini kuwa kwa umoja wenu na kwa ushirikiano na viongozi pamoja na watumishi wengine wa TAKUKURU mtaisaidia Serikali anayoiongoza kuijenga Tanzania ambayo wananchi wake watanufaika na rasilimali za umma na kupata huduma bora pasipo kuombwa au kutoa rushwa,


Tumieni nafasi hii kujenga nguzo kuu za serikali za kuinua na kukweza ufanisi wa uwajibikaji uwe na watumishi wa umma wenye miiko ya maadili kwa ustawi na maendeleo ya jamii na Taifa, taasisi hii ni nanga ya Taifa letu kwa usalama wa tija ya kutoa wajibu wa uwazi na ukweli wa kuchangia utawala bora, mkizembea tunaanguka wote na mkiwa imara na kutimiza wajibu wenu ipasavyo, tunainuka wote,"amesema Mchengerwa.

Pamoja na hayo amewataka watumishi wa Taasisi hiyo kuacha woga na kutambua kuwa wao ni kioo cha jamii hivyo matendo yao yanapaswa kuwa safi .

“Wito wangu kwenu ni kwamba tathmini yetu iwe ya kina na tutazame namna tutakavyoweza kujipambanua katika kila Wilaya namna bora ya utendaji”, amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salumu Hamduni,amesema wametekeleza majukumu na kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla ya shilingi billion 29.3 ziliokolewa na kwamba billion 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslim na utaifishaji mali na kiasi cha bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.

Ameeleza miradi ya kimaendeleo 1,188 yenye thamani ya bilioni 714.17 katika sekta ya afya maji elimu ziliweza kufatiliwa na kuona makosa ambayo wameyachukulia hatua.

“Tumeelimisha katika ngazi ya Makao Makuu pamoja na wakuu wa TAKUKURU, kuzuia vitendo vya rushwa kuelimisha, kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watuhumiwa Mahakami kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya mashtaka ambapo majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa na majadala 339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakani ambapo kesi mpya zilipatikana 542, na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345”,amesema Hamduni

Kutokana na hali hiyo amesema wao wakiwa na dhamana ya kupinga masuala ya rushwa nchini wataendeleza juhudi kuelimisha umma kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kuzuia mianya ya rushwa.

"Tunatambua wapo wananchi ambao hawajafikiwa,tunaendeleza jitihada za kuwafikia wananchi na hasa waliopo vijijini n kuendelea kutoa kipaumbele zaidi katika kuzuia vitendo vya Rushwa ikiwemo kuwaelimisha wananchi ili wafahamu haki zao katika upatikanaji wa huduma, madhara ya rushwa na jinsi ya kutoa taarifa za rushwa,"amefafanua Hamduni.

Mbali na hayo ameeleza kuwa Taasisi hiyo ina wajibu sahihi usiopoka haki za wasio na kasoro za kupata haki za Uhuru wa dhamana na kwamba hakimu haki ndiye atajenga sifa nzuri za kuthaminika nyinyi ni taasisi ya utalawa Bora kwa Serikali ya awamu ya sita.

" Ni imani yetu kuwa wananchi wakiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Rushwa na madhara yake basi itawarahisishia kukabliana nayo kwakuwa hawatatoa wala hawata sita kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa,elimu hiyo itawafunua zaidi macho wananchi, kutambua vitendo vya rushwa vinavyoweza kutokea katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutoa taarifa kwenu na kwa mamlaka nyingine zinazohusika,"ameeleza Mtendaji huyo Mkuu wa TAKUKURU nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments