MIAKA 60 YA UHURU , MINARA YA MAWASILIANO YAZIDI KUJENGWA


Dkt. Ashatu Kijaji

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog DODOMA.

SERIKALI kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF)  imejenga minara 1,068 kwa kutumia ruzuku ya Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma ambapo hadi sasa takribani shilingi bilioni 161 zimetumika kujenga minara hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jijini hapa na Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji  wakati  akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari  kuhusu mchango wa Sekta hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania huku akieleza majukumu ya Wizara hiyo kuwa yamepitia mabadiliko mbalimbali ya kuundwa kwake, kabla na baada ya Uhuru.  
 
 Ameleeza  kuwa, ujenzi wa minara ya mawasiliano umefanyika kwenye kata 2,579 za Tanzania Bara kati ya kata 3,956 ambazo ni sawa na asilimia 65 na kwa upande wa Zanzibar, minara hiyo imejengwa kwenye kata 101 kati ya kata 110 ambazo ni sawa na asilimia 92. 

"Mnara mmoja una uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano kutoka eneo mnara ulipo hadi eneo la umbali wa kilomita 11 kutegemea na jiografia ya eneo husika na aina ya masafa kwa kuwa huduma za mawasiliano kutoka katika mnara zinafika mbali zaidi kama eneo ni tambarare, halina misitu, miti mirefu, miinuko na milima,"amefafanua. 
 
Mbali na hayo Serikali katika azma yake ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya mawasiliano ya uhakika na kwa gharama nafuu, Dkt.Kijaji amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, umetangaza zabuni ya shilingi bilioni 37.7 za ujenzi wa minara 224 ya mawasiliano katika maeneo ya kimkakati na mipakani.

Amefafanua kuwa mfuko huo umehuisha teknolojia zilizokuwa zikitumika kwenye baadhi ya minara ambazo zilikuwa zina uwezo wa 2G kwenda kwenye teknolojia ya 3G na 4G; kufikisha huduma ya mawasiliano kwenye halmashauri kumi nchini ambazo ni halmashauri ya Mbogwe, Tanganyika, Kakonko, Malinyi, Mtwara Vijijini, Msala Vijijini, Pangani, Bariadi, Nzega na Kilindi. 

"Lengo likiwa kila mwananchi aweze kupata huduma za intaneti bila kujali yupo mjini au vijijini kwa sababu huduma ya intaneti ni huduma ya msingi kama ilivyo huduma ya mawasiliano ya simu ambayo kila mwananchi ana haki ya kupata huduma ya intaneti,mfuko huo  unatarajia kutangaza zabuni za huduma ya mawasiliano ya redio zenye jumla ya shilingi bilioni 1.5 kwa lengo la kuboresha mawasiliano ya redio ili kuongeza wigo wa wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati,"amefafanua. 

Kwa upande wa huduma za Posta Nchini,amesema Serikali kupitia Wizara hiyo  imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za Shirika la Posta Tanzania kutoka kutoa huduma za barua na kupiga simu za mezani mpaka Shirika kuanza kutoa huduma zake kwa njia ya kidijitali kwa kuanzisha huduma mbalimbali kama posta mlangoni, posta kiganjani ambapo laini ya simu ya mteja ndiyo sanduku lake la barua.

Ameongeza kuwa huduma za duka la posta mtandao zimeendelea kupanua wigo wa usafirishaji wa mizigo, barua na vipeto na kusaidia shirika hilo kuanzisha mashirikiano na taasisi mbalimbali za Serikali kwa kuanzisha huduma za uwakala ambapo mpaka sasa Shirika la Posta ni wakala wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Benki za CRDB na NBC, Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC). 

"Kwa kazi njema ambayo Shirika la Posta Tanzania linafanya, 15/11/2021 shirika limekabidhiwa kifimbo cha Malkia (Queens Baton Relay) na kamati ya Olympic Tanzania kwa ajili ya kusafirishwa na Shirika kwenda sehemu mbalimbali Duniani!!! Nawakaribisha sana Watanzania ili tuendelee kutumia huduma za Shirika letu la Posta ambazo zimeboreshwa sana,"amesisitiza Waziri huyo.
 
Kadhalika amesema ili kuiandaa nchi kwa mabadiliko ya Kiteknolojia na uchumi imara katika Miaka Miaka 60 ijayo, serikali inaendelea kuwekeza na kuweka vipaumbele mbalimbali ikiwemo kukuza Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA ambapo hatua za awali zilizofanywa na Serikali ni kuboresha uratibu kwa kuziweka sekta hizi chini ya usimamizi wa Wizara moja ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na uendelezaji wa sekta hizi nchini. 
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments