TUME YA HAKI ZA BINADAMU KUANZA KUSIKILIZA MALALAMIKO 561 MIKOANI


 Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB Nabor B.Assey akiongea na Waandishi wa habari kuhusu ziara ya tume hiyo inayolenga kusikikiza malalamiko ya wananchi.

****

Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

TUME ya haki za binadamu na utawala bora (THBUB)inatarajia kuanza ziara ya kuimarisha uhusiano wake na Jamii katika utendaji kazi kwa kuyatafutia ufumbuzi malalamiko 561 ya wananchi na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora kwa wananchi.


Hayo yameelezwa jana Novemba 19,2021 Jijini hapa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Nabor B.Assey wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu ziara ya kutembelea mikoa 24 nchini ili kuzungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali Selikalini,Asasi za kiraia(AZAKI)na kufuatilia  malalamiko  ya wananchi ambayo yamewasilishwa kwenye tume hiyo. 


Ameyataja baadhi ya malalamiko ambayo yanaripotiwa kwenye tume hiyo ni pamoja na uvunjifu wa haki za binadamu,ukiukwaji wa utawala bora ,ajira,ardhi,mapunjo ya stahiki za kustaafu ,kubambikiwa kesi na uchelewashaji wa kesi ambapo mara nyingi walalamikiwa huwa ni watendaji wa Serikali.


"Ziara hiyo itafanyika Novemba 22 hadi 26,2021 lengo ni kuimarisha mahusiano na kutambulisha kazi zetu kwa jamii,katika ziara hiyo ambayo itaongozwa na makamishna na maafisa waandamizi,tutakutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa sekretarieti za mikoa mitano Tanzania bara na mitano visiwani,"amesema na kuongeza;


Mikoa hiyo ni Dodoma,Kigoma,Kagera,Tanga na Lindi na kwa upande wa Zanzibar ni Mjini Magharibi,Kaskazini Unguja,Kusini Unguja,Kaskazini Pemba na Kusini Pemba vile vile kuna mikoa mingine itakayotembelewa katika ziara hii ni Dar Es Salaam,Morogoro ,Singida ,Arusha ,Mtwara ,Ruvuma,Iringa ,Mbeya ,Songwe ,Tabora ,Shinyanga ,Mwanza ,Mara na Geita,"amefafanua.


Kaimu Katibu Mtendaji huyo wa THBUB ameeleza kuwa hatua hiyo itakuwa ni ya pili ambapo katika awamu ya kwanza iliyofanyika Septemba 7 hadi 9,2020 Tume hiyo ilifanya mazungumzo na Sekretarieti za mikoa sita ya Tanzania bara na kamati za ulinzi na usalama za mikoa mitatu ya Zanzibar.


"Awamu ya kwanza ilihusisha mikoa ya Arusha,Tabora,Mwanza,Dar Es Salaam,Mbeya na Morogoro na Kwa upande wa Zanzibar ni Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja na Kusini Unguja,"amesema


Zaidi ya hayo ameeleza kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango mkakati wa THBUB wa Mika mitano kuanzia 2018/2019-2022/2023 ambao miongoni mwa malengo yake ni kulinda na kukuza haki za binadamu na misingi ya utawala bora.


"Kutokana na ziara hii tunaamini itasaidia viongozi hususani wa Serikali za mitaa,AZAKI na wananchi wengi zaidi kuifahamu THBUB,kazi zake na huduma inazotoa ikiwa ni pamoja na kutambua haki na wajibu wao, mifumo iliyopo ya kudai haki na wananchi wengi watapata nafuu ya malalamiko yao,"amesisitiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments