RBA - INITIATIVE KUCHUKUA HATUA ZAIDI KUENDELEA KUPAMBANA NA TATIZO LA USUGU WA VIMELEA


Na Dotto Kwilasa, DODOMA.


IKIWA ni wiki ya kuongeza uelewa kuhusu vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa duniani, shirika lisilo la kiserikali la RBA-INITIATIVE linalojikita kupambana na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa Jijini Dodoma limesema kuwa linaendeleza kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na tatizo hilo ikiwemo kutoa elimu kwa makundi maalum.


Hayo yamebainishwa Jijini hapa na Mfamasia kijana ambaye pia ni mwanzilishi na mtendaji mkuu wa shirika
hilo Erick Venant wakati
akizungumza na madereva bajaji ambao ni Mabalozi wa kampeni ya kujenga uelewa na kuzingatia matumizi sahihi ya dawa .


Amesema,katika kuadhimisha wiki hiyo wao kama wadau wa afya huadhimisha kila mwaka ambapo kwa mwaka huu wametilia maanani katika kuandaa kampeni maalum na mafunzo ya kujenga uelewa na kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kwa madereva bajaji na waandishi wa habari mkoa wa Dodoma,ili kufikisha ujumbe kwenye jamii .


Hata hivyo amesema,pamoja na jitihada zote hizo hali bado mbaya ambapo takribani watu laki saba duniani kote hupoteza maisha kutokana na usugu huo na kwamba endapo hatua za ziada hazitachukuliwa vifo hivi vinaweza kufikia watu millioni 10 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050 .


"RBA-INITIATIVE tunaongeza jitihada kupambana na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa,Kwa mwaka huu tunaongeza zaidi wigo wa mapamano,jamii inapaswa kufahamu tatizo bado linahiaji nguvu ili kuiweka jamii salama,"amesema Venant.


Naye Mkurugenzi Msaidizi,Ofisi ya Waziri Mkuu,kitengo cha maafa Dkt. Charles Msangi Serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kiserikali katika kuteleza mpango mkakati wa usugu wa vimelea vya usugu wa magonjwa wa mwaka 2017/2022 kwa kuzingatia dhana ya AFYA MOJA.


Msangi amesema usugu ya vimelea vya magonjwa hutokea pale ambapo virusi vya vimelea hivyo kushindwa kutibika hususani kwa dawa maalumu na kusababisha kuongeza kasi kwa magonjwa na makali ya ugonjwa na kupelekea vifo vingi kwa watu.


Amesema usugu huo wa vimelea vya magonjwa unahitaji wataalamu katika sekta mbalimbali kuweza kufanya kazi kwa pamoja ili kushughulikia kwa kasi suala hilo kwani kumekuwa na kasumba duniani juu ya suala hilo ambalo husababisha vifo katika mataifa mbalimbali duniani.


Aidha amewataka wadau wa mazingira kuhakikisha wanaendelea kuchukua taadhari juu ya suala hilo kwani vimelea vingi hutoka kwa mifugo inayofugwa majumbani na kuwadhuru binadamu huku akieleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uratibu wa masuala ya Afya moja, ambayo ni dhana inayo jumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo, kilimo na mazingira kushirikiana kwa pamoja katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu.


Zaidi ya hayo amesisitiza kuwa Ofisi hiyo kwa kushirikiana na shirika la RBA Initiative itaendeleza dhana hiyo kwa kuwa inapunguza gharama katika kushughulikia athari za usugu wa vimelea vya magonjwa ambavyo husababishwa na hali ya dawa kushindwa kudhibiti vimelea hivyo kwa kushindwa kabisa kuviua au kuzuia ukuaji wake.


“Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na Kimataifa ni kujiandaa kwa kufundisha wataalam wa sekta za afya na wadau wa Afya moja jinsi ya kufanya tathmini ya hatari ya vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kwa ushirikiano,katika kutekeleza haya yote tunapaswa kushirikiana,"amesema.


Wiki ya kuongeza uelewa kuhusu usugu wa vimelea kwa vijiuasumu(Antibiotics) duniani huadhimishwa mwezi Novemba kila mwaka duniani ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu usugu wa vimelea kwa vijiuasumu, maadhimisho haya kwa mwaka huu 2021 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo " Eneza ujumbe ,zuia usugu wa vimelea vya magonjwa" .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments