WATU WAWILI WAFARIKI AJALI YA BASI LA KIMOTICO ARUSHA

Basi la Kimotico likiwa limepinduka

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha
Watu wawili wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya Basi na T536 CYC aina YUTONG Kampuni ya Kimotico kuacha njia na kupinduka katika barabara ya Arusha-Babati, eneo la Makuyuni wilayani Monduli mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema tukio hilo limetokea leo Oktoba 26,2021 majira ya saa moja asubuhi maeneo ya Mbuyuni Makuyuni karibu na mzani ambapo Basi lenye namba za usajili T536 CYC aina YUTONG Kampuni ya Kimotico ambayo inafanya safari zake Arusha kwenda Musoma likiendeshwa na Omary Ally iliacha njia na kupinduka kitendo kilichopelekea kupoteza maisha ya watu wawili.

Kamanda Masejo amesema majeruhi katika ajali hiyo walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru Mkoani Arusha kwa matibabu zaidi.

Aidha Kamanda Masejo amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru kwa utambuzi zaidi.

Amewataka madereva kuzingatia alama za usalama barabarani sanjari na ukarabati wa mara kwa mara wa magari yao ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments