MRADI WA HPSS WAFUNGA OFISI ZAKE ZA KANDA UKIWA BADO UNAHITAJIKA

Na Jackline Lolah Minja - Morogoro
Mradi wa Tuimarishe Afya (HPSS) ambao umekuwa ni mdau mkubwa katika Sekta ya Afya hapa nchini umefunga Ofisi zake za Kanda nakubakiza Ofisi za HPSS Taifa huku ikielezwa kuwa mradi huo bado unahitajika hususani wakati huu ambapo Serikali inaelekea kuanzisha Bima ya Afya kwa wote kipindi kifupi kijacho.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt. Gunini Kamba wakati wa kikao cha kufunga Ofisi za Mradi wa  HPSS Kanda ya Mashariki kilichofanyika Oktoba 22 mwaka huu katika hoteli ya Glonency iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Dkt. Kamba amesema pamoja na kuwapongeza HPSS kwa kazi nzuri walizofanya kwa kipindi kifupi ikiwemo kuongeza usajiri kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii - ICHF, masuala ya usambazaji na menejimenti ya dawa – JAZIA, na kazi nyingine nyingi bado Mradi huo ulikuwa unahitajika katika kanda hiyo ya Mashariki husuan katika kipindi hiki ambacho Serikali inataka kuanzisha Bima ya Afya kwa kila mwananchi.

“Kuna mambo ambayo tulikuwa tunaendelea kuyajenga, ukizingatia Serikali inelekea kuanzisha bima ya Afya kwa wote, kila mwananchi atatakiwa apate Bima ya Afya, sasa nao ndipo wanaondoka, tulitaraji huu mswada ambao utapitishwa mwezi ujao Novemba labda tungeweza kukubaliana nao kusaidia kwenye suala la Bima ya Afya kwa kila Mwananchi”, alisema Dkt. Kamba.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira amewataka Wajumbe wa kikao hicho kuendeleza yote mazuri yaliyoazishwa na Mradi wa HPSS huku akiamini kwamba hilo linawezekana kwa kuwa viongozi wa mradi huo walifanya kazi kwa kushirikisha wajumbe wa RHMT wa Mikoa yote husika ya Dar, es Salaam, Pwani na Morogoro.

Aidha amesema, ipo kasumba hapa nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro miradi inayoaazishwa kukosa mwendelezo wake, baada ya mradi kuanzishwa na mradi unapofika kikomo cha ufadhiri, mradi nao unakufa na kwamba hangependa hilo litokee ndani ya mikoa hiyo ya Kanda ya Mashariki.

Badala yake amewataka wajumbe wa kikao hicho kuendele kufanya mawasiliano na Viongozi wa HPSS wa Ofisi za Taifa ili kama kuna jambo halikukamilika au kueleweka yafanyike mawasiliano na Ofisi hizo zilizopo Jijini Dodoma ili kupata ufafanuzi wa jambo hilo lengo ikiwa ni kuendeleza kazi za utoaji wa huduma ya Afya kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.

“Kuna kawaida miradi mingi inayoanzishwa nchini kwetu, hata hapa Morogoro inakuwa haina mwendelezo, mradi unaanza ukifika mwisho inakuwa ndio mwisho wa maradi. Lakini mimi naamini kwenye mradi huu kwa kuwa kulikuwa na ushirikishwaji na timu za RHMT na wadau wengine mradi huu utakuwa ni endelevu”, alisema Dkt. Rozalia

Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa - ICHF Mkoa wa Morogoro Alicia Mtesigwa, amekiri kuwa HPSS kama Mdau wa Afya, wamekuwa na mchango mkubwa katika Afua ya ICHF hususan katika uandikishaji, uhamasishaji na utoaji wa huduma za Bima hiyo kwa ngazi zote na kwa Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Morogoro.

Hata hivyo Bi. Alicia amebainisha mikakati waliyoiweka baada ya kutambua kuwa mradi unakwenda kufika kikomo, lengo ni kuendeleza yote mazuri yaliyofanywa na HPSS bila kutetereka kwa kutenga bajeti kwa kila Halmashauri kwa ajili ya shughuli hizo zilizokuwa zinafanywa na HPSS.

Akitoa taarifa ya kufunga Mradi wa HPSS kanda ya Mashariki na kubakiwa na Ofisi ya HPSS Taifa pekee ambayo itakuwa Jiji la Dodoma, Afisa wa HPSS wa kanda hiyo Bi. Alice Mwashilindi amesema Mradi wa HPSS ulikuwa unasaidia katika maeneo manne yaani uhamasishaji wa mfuko wa Bima ya Afya ulioboreshwa – ICHF, Uhamasishaji wa Afya Kinga, na kushughulikia mfumo wa usambaza madawa na menejimenti yake unaofahamika kama JAZIA katika maeneo ya kutolea huduma za Afya kama Hospitali na Vituo vya Afya.

Hata hivyo Bi. Alice amesema Mradi wa HPSS unapoelekea kufungwa kiutendaji katika Kanda hiyo yenye mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro anaamini kazi zilizoanzishwa na HPSS zitakwenda kuimarishwa na kuendelezwa kwa kuwa walifanya kazi kwa kushirikisha timu za kila Halmashauri na kwamba wataweza kwa sababu timu hizo zina muundo mzuri.

 “Tumeweza kuwajengea uwezo mkubwa kabisa, kwa hiyo mpaka sasa tunaondoka kwenye ofisi zetu za kanda tukiwa na uhakika kabisa kwamba timu zetu za mikoa zina uwezo mkubwa wa kuzifanya zile shughuli walizokuwa wanazifanya kwa sababu tayari tumekwisha zijengea uwezo”, alisema Bi. Alice. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments