TAMASHA LA ZIFF KURINDIMA TANZANIA BARA



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

TAMASHA la Kimataifa la Filamu za Nchi Majahazi (ZIFF), ambalo ufanyika kila mwaka  mwezi wa Juni/Julai kwa sasa linatarajiwa kufanyika Tanzania Bara katika vituo kadha kuanzia tarehe 28 Oktoba mwaka huu.

Tayari Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) hapa nchini mapema leo 26 Oktoba wamezindua rasmi kuelekea kwa maonesho ya filamu kwa uratibu wa ZIFF kwa ushirikiano na Ubalozi wa Nchi za Ulaya.

Ambapo ZIFF imetayarisha maonesho hayo maalum ya filamu zilizoshinda tuzo za  ZIFF mwaka huu pamoja na filamu adhimu toka nchi mbalimbali za Ulaya. 

Filamu hizo za nchi za Ulaya ni pamoja na filamu toka Hispania, Italia, Ubeligiji, Ujerumani, Ufaransa, Swiden, Finland na Poland.

Akizungumzia tamasha hili la mwezi mzima Balozi wa Nchi za Ulaya, Bwana Manfredo  Fanti alisema kuwa,  ZIFF ni kiungo muhimu kati ya tamaduni za dunia kupitia uoneshaji wa filamu. 

"Filamu ni sehemu muhimu ya kuwasiliana kimataifa, kuelimisha jamii na ajira, hasa kwa vijana. Tunashirikiana na ZIFF kupanua wigo wa taaluma ya filamu hapa nchini kupitia mafunzo na maonesho kama haya," aliongezea.

Tamasha litafanyika katika vituo vinne ambavyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Mwanza, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (Tasuba). 

Kila wikiendi kwa mwezi mzima zitaoneshwa filamu katika kituo kimojawapo ili kukaribisha hadhira kuona filamu toka nchi za Ulaya na zile ambazo zimeshinda au kuoneshwa katika Tamasha la ZIFF mwaka huu.

“Kwa kuonesha filamu zilizoshinda katika tamasha la ZIFF tutaweza kuwaonesha watengenezaji wa  filamu wa Tanzania filamu zenye viwango vya kimataifa na kwa njia hiyo kuwawezesha kujipima wenyewe.” Alisema Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF Profesa Martin Mhando.

Aidha, Tamasha hilo litafunguliwa tarehe 28 Oktoba majira ya jioni katika Ukumbi wa Taasisi ya Utamaduni ya Ufaransa ya Dar-Alliance Francaise  iliyopo Upanga Dar es Salaam. 

Filamu itakayofungua dimba la tamasha hilo ni filamu ya  'Binti' iliyotengenezwa na Mtanzania, Bi Seko Shamte.

Wadau wa filamu mbalimbali wamekaribishwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia filamu hizo zenye kuburudisha, kuelimisha na kutoa mafunzo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments