JESHI LA WANANCHI TANZANIA 'JWTZ' KUSAMBAZA VITABU ZAIDI YA MILIONI 20 AWAMU YA KWANZA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Friday, October 15, 2021

JESHI LA WANANCHI TANZANIA 'JWTZ' KUSAMBAZA VITABU ZAIDI YA MILIONI 20 AWAMU YA KWANZA


Waziri Prof Ndalichako  (katikati) wakionesha  vitabu vitakavyosambazwa na jeshi la Wananchi Tanzania  (JWTZ) wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam
Waziri Prof Ndalichako akikagua moja ya kitabu kwenye gala la vitabu vinavyosimamiwa na Taasisi ya elimu Tanzania  (TET)

Na Andrew Chale -Dar es salaam

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Prof. Joyce Ndalichako amelishukuru Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kuendelea kushirikiana na Wizara yake ikiwemo suala la usambazaji wa vitabu zaidi ya milioni 20.9 ambavyo vitapelekwa Halmashauri zote Nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo rasmi Jijini Dar es Salaam, Waziri Prof. Ndalichako alisema vitabu hivyo vitakavyoenda Halmashauri zote ni pamoja na vile vya elimu ya awali, msingi, kundirika la kwanza mwaka (¡&¡¡), Maandishi yaliyokuzwa na Sekondari.

"Leo tupo hapa kuzindua rasmi zoezi la usambazaji awamu ya kwanza na jeshi letu la Wananchi ndiyo limepewa jukumu.

Namshukuru sana Mkuu wa Majeshi CDF Mabeyo kwani kwa sasa jeshi la Wananchi limekuwa kweli la Wananchi kila tunapowaitaji wanakuwa na sisi. Tunawapongeza sana kuona ushirikiano wanaotupatia" Alisema Waziri Prof. Ndalichako. 

Waziri Prof. Ndalichako pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  (JMT), Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha pesa ambazo zimesaidia machapisho hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi na wabia.

"Fedha za Serikali na wadau zaidi ya Bilioni 46.4 zimewezesha machapisho haya ambayo kwa awamu hii ya kwanza yataenda Halmashauri zote Tanzania Bara na pia Visiwani.

Vitabu hivi milioni 20 ni kwa uwiano wa kitabu kimoja wanafunzi wawili lakini mzazi ruksa kununua kitabu kwa mwanao. Muje hapa utakinunua", alisema Waziri Prof. Ndalichako.

Aidha, alisema vitabu hivyo taasisi ya elimu Tanzania wameviandaa kwa kuzingatoa ubora na vitamsaidia mwanafunzi kupenda kusoma na kujifunza.

"Vitabu vitamuongoza mwalimu kwa kila topiki ya kusomea. Kwa hiyo mwanafunzi anaweza kusoma vitabu hivi na mwisho kuna majaribio yanayopatikana kwa kila kitabu." Alisema na Waziri Prof. Ndalichako  na kuongeza:

"Utamaduni wa kujisomea hapa kwetu bado upo chini. Tunataka tuwe na utamaduni wa kujisomea hata ukimaliza shule. Kwa sasa tuna vitabu vya kila aina, hata kama utasoma hadithi ni kujiimarisha kusoma...vitabu hivi vitamuezesha mwanafunzi kuumudu mazingira katika maisha yake." alisema Waziri Prof. Ndalichako. 

Aidha, Waziri Prof. Ndalichako alituma salamu za Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu ambapo aliagiza vitabu hivyo vitakapofika kwenye Halmashauri viende moja kwa moja mashuleni na vikatumike na si kufungiwa stoo ili kuogopa kuchafuka.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa TET, Dk Aneth Komba amesema wataendelea na kazi ya uandishi na uchapishaji kwa kutumia wataalam taasisi hiyo na wabobezi wa vyuo, wastaafu na taasisi binafsi ilikukuza elimu hapa nchini.

Aidha, amemuhakikishia Waziri Prof.  Ndalichako kuwa vitabu hivyo vitasambazwa kwa ngazi zote ikiwemo ya Halmashauri ambapo maafisa watajaza fomu kupitia simu janja zao.

" TET itaona vitabu vyote kupitia mfumo kutoka kwa maafisa wote watakaotumia simu janja zao hivyo vitabu vitafika na kuonekana kwenye mfumo rasmi." alisema Dkt. Aneth Komba.

Naye Kanali Benjamini Kisinda wa jeshi la Wananchi Tanzania, alisema kama jeshi limejipanga kufanya zoezi hilo kwa weledi mkubwa na kutimiza majukumu hayo ya kitaifa.

"Tunashukuru sana kwa imani kwa jeshi letu na sisi tunaahidi kuvifikisha vitabu hivi sehemu husika na wakati sahihi. Tunashukuru kwa kuendelea kuwa na imani na jeshi asanteni sana", alisema Kanali Benjamin Kisinda.

Awali kabla ya uzinduzi huo, Waziri Prof. Ndalichako alipata wasaha wa kukagua gala la vitabu hivyo ambavyo vinasubiria kusafirishwa nchini kote ambapo alilidhishwa na ufanisi mkubwa uliofanywa na taasisi ya elimu Tanzania  na kuweza kuandaa vitabu hivyo huku akitoa rai kuwa endapo kutatakiwa vitabu zaidi wadau wanaweza kutoa maoni yao na wao kama Wizara wataona namna ya kuandaa.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages