Breaking News: OLE SABAYA NA WENZAKE WATUPWA JELA MIAKA 30


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake baada ya kukutwa na hatia ya unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo amesema kuwa ameridhika mashtaka dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake na kuwatia hatiani kosa unyang’anyi wa kutumia silaha.

Baada ya kuwatia hatiani wakili wa Serikali amesema hakuna kumbukumbu ya makosa ya zamani ya washtakiwa wote watatu, na kuiomba Mahakama iwape adhabu ya miaka isiyopungua miaka 30 jela na viboko.

Hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha iliyokuwa ikimkabili Sabaya imesomwa leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo.

Kabla ya kuanza kusomwa hukumu, Wakili wa Serikali, Felix Kwetukia aliweka wazi kuwa Jamhuri ipo tayari kupokea hukumu huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Moses Mahuna, Silvester Kahunduka na Wakili Fridolin Germelo nao walisema wapo tayari kusikiliza hukumu hiyo.

Hakimu Omworo amesema kuwa imethibitika mshitakiwa wa kwanza alikuwa na bastola ndani na nje kulikuwa na watu wawili wenye silaha hivyo, hakuna shaka duka la shahidi wa kwanza lilivamiwa na watu wenye silaha na lilikuwa chini ya watu wenye silaha.

Washtakiwa, Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani leo saa 3:05 asubuhi, kwa ajili ya hukumu ambapo Oktoba 1 2021 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo kwa maelezo ya kutokamilisha kuandika hukumu hiyo.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka huu baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Lengai Ole Sabaya amezaliwa 26/12/1986 mkoani Arusha. Amesoma Shahada ya Sayansi katika Elimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu John Dodoma (St. John University).

Ole Sabaya aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha na pia aliwahi kushika wadhifa wa Udiwani katika kata ya Sambasha Wilaya ya Arusha Mjini mwaka 2015.

Ole Sabaya aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro tarehe 28 Julai 2018 ya aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli.

Sabaya alitenguliwa nafasi hiyo ya ukuu wa Wilaya ya Hai tarehe 13 Mei 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan ili kupisha uchunguzi wa makosa yaliyokuwa yakimkabili ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha.

Tarehe 15 Oktoba 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha imemhukumu Sabaya na wenzake kifungo cha miaka 30 jela.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments