WAMACHINGA MOROGORO WATAKIWA KUKUZA BIASHARA ZAO NA KUTUNZA VIBANDA WALIVYOPEWA


Na Jackline Lolah Minja - Morogoro
Wafanyabiashara wa biashara ndogo (machinga) wilaya ya Morogoro wametakiwa kuhakikisha wanakuza biashara zao pamoja na kutunza vibanda walivyopewa ili kupunguza wimbi la vijana kukosa ajira na kuufanya mji wa Morogoro kuwa safi.

Akizungumza na wafanya biashara hao katika hafla ya uzinduzi wa vibanda hivyo ambayo imehudhuriwa na mkuu wa mkoa wa morogoro Martine Shigella ,Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu, pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara  Profesa Kitila Mkumbo ,Mkuu wa wilaya ya Morogoro Alberto Msando amesema lengo la vibanda hivyo ni kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakuza mitaji yao na kuongeza uchumi kwa nchi ,hivyo wahakikishe wanalinda na kudumisha amani upendo pamoja na heshima waliyopewa kwa maslahi ya nchi na jamii kwa ujumla.

“Ni lazima tuthamini utu wa kila mmoja wetu, na sisi kama viongozi tunawajibu wa kutambua kwamba kila mwananchi raia wa Tanzania anao utu wake lazima kuuthamini bila kujali anachokifanya kwa kuwa havunji sheria na anapata kipato halali na kwa kutambua hilo ndiyo maana tunakaa na machinga tunakula nao tunacheka nao na sasa wako tayari kushirikiana na sisi ilimradi kila mtu afikie lengo lililo kusudiwa”, alisema Msando.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela amewataka wafanyabiashara hao kutoweka tofauti kati ya viongozi na kusababisha mgawanyiko baina ya viongozi wa mkoa huo.

“Na hakuna sababu ya kugawanyika kwenye suala la maendeleo, niwaombe sana wamachinga na wafanyabiashara wa Morogoro sisi sote ni viongozi wenu wala msishiriki mahala popote kututengenezea mgawanyiko kwa kuwa sisi tunawahudumia nyinyi ,kila mmoja anamchango wake,kwahiyo hakuna sababu”alisema Shigela.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amesema katika sera ya biashara inatambua biashara ndogo na biashara zingine hivyo mkoa wa Morogoro utakuwa ni sehemu ya kujifunza hasa kwenye upande wa upangaji biashara umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Tumefika hapa serikali inapozungumzia kuunga mkono biashara ndogo kutokana na sera inavyosema hakuna mfanyabiashara mdogo bali ni mfanyabiashara wabiashara ndogo,na hivyo tumekuja kujifunza na ni waambie kwa hili mlilolifanya Morogoro mmekuwa ni shule ya kujifunza afrika nzima kwakuwa tatizo la machinga ni la Afrika nzima hivyo nitawaalika viongozi wengine wa biashara wa Afrika waje kujifunza hapa ili kuweza kuondokana na tatizo hili,kwa hiyo mimi niwapongeze tu viongozi wa mkoa huu”, alisema Profesa Mkumbo.

Hata hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  Ummy Mwalimu amesema ni wakati wa viongozi kuhakikisha wanatatua changamoto zilizobaki kwa wafanyabishara hao kwa kutafuta namna ya kuwafikia hata kwa kuanzisha machinga day kwaajili ya kukusanya wamachinga ili kuwapa elimu mbalimbali za kufanya biashara.

“Niagize hili kwa kila halmashauri ,muhimu sana viongozi wenzangu kuwa na vikao na hawa machinga hata mara mbili kwa mwaka ili kujadili maendeleo ya machinga na si vibaya mkaja na machinga day hii ni kwaajili ya kukaa nao walete changamoto zao,kupeana elimu ya ujasiliamali na kutunza fedha,na waeleze maono yao na mikakati yao ili tujue nini cha kufanya na kutekeleza majukumu yao”, alisema Ummy.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments