TECMN YAOMBA SERIKALI, JAMII NA WADAU KUONGEZA JUHUDI ZA KUTOKOMEZA NDOA ZA UTOTONI

Na Magreth Katengu - Dar es salaam
Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania (TECMN) umeiomba serikali,jamii na wadau wote wa maendeleo kuongeza juhudi za pamoja kuhakikisha suala la ndoa za utotoni linatokomezwa ili kusaidia kujenga kizazi kijacho chenye usawa wa kiuchumi.

Ombi hilo limetolea Jijini Dar es salaam na Mratibu Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Euphomia Edward  katika kikao kazi  kilichojumuisha Mashirika yasiyo ya kiserikali 64 ambapo amesema kwa mujibu wa takwimu kutoka  utafiti wa Demografiana afya Tanzania wa mwaka 2015/2016 zinaonyesha  asilimia 36 ya wasichana  wenye umri kati ya miaka 20_24  waliolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Hata hivyo amesema pamoja jitihada zote zinazofanywa na Mashirika hayo wamekua wakiwasaidia baadhi ya wahanga kiuchumi kwa kuwapatia mitaji na ujuzi katika fani mbambali ili wajikwamue na umasikini uliosababisha hadi wazazi wao wakawaozesha wangali wadogo

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shinyanga Mustapha Sebuja amesema ndoa za utotoni husababishwa na umaskini,mila potofu, desturi,ukosefu wa elimu ,mapungufu katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 sheria hii wadau na serikali wangekaa na kuifanyiia marekebisho

"Ni kweli kabisa mkoa wa Shinyanga ndio mkoa unaoongoza kwa ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ukifuatiwa na Tabora asilimia 58 Mara asilimia 55 huku Dodoma ukiwa asilimia 51 hali hii ya mikoa hii ni hatari sana kwa watoto wa kike wanaotokea katika jamii hizi ni budi serikali na wadau wengine kuongeza jitihada za makusudi kutokomeza suala hili", alisema Sebuja.

Naye Mwakilishi kutoka Tabora Mayaya Marko amesema watoto wa kike wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18 wanakumbana na changamoto ya kupoteza fursa ya elimu,kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa ya zinaa,kuteseka kisaikolojia ,kuyumba kiuchumi,kuwa katika hatari kubwa kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia

Aidha wito umetolewa kwa watu watu wote kutoa ushirikiano Kwa vyombo vya sheria pale wanapoona viashiria vya kuozeshwa mtoto   wa kike aliye chini ya umri wa miaka 18 .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post