TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO KATIKA MAONESHO YA BIASHARA YA AFRIKA MASHARIKI YANAYOENDELEA JIJINI MWANZA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, September 5, 2021

TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO KATIKA MAONESHO YA BIASHARA YA AFRIKA MASHARIKI YANAYOENDELEA JIJINI MWANZA


Afisa Usalama wa Chakula, Donald Mkonyi akitoa elimu kwa wadau waliotembelea banda la TBS katika maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyofanyika mkoani Mwanza. TBS imetumia fursa hii kutoa elimu ya Viwango kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla.

****************************

WAFANYABIASHARA na wajasiriamali wa mikoa ya kanda ya ziwa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha na kusajili majengo na bidhaa za chakula na vipodozi ili kuondokana na vikwazo vya kibiashara ndani na nje ya nchi.

Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Afisa Masoko wa TBS, Deborah Haule, wakati akizungumza na washiriki na wananchi waliotembelea maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyofanyika kuanzia Agosti 27, mwaka huu na kumalizika jana Septemba 5, jijini Mwanza.

Haule alisema, TBS imeshiriki katika maonesho haya kwa lengo la kuwasogezea huduma karibu wajasiriamali na wafanyabiashara kwa ujumla na kutoa elimu ya viwango ili waweze kuzalisha bidhaa bora na salama zinazoweza kushindana katika soko la kimataifa.

“Nchi za Afrika Mashariki zina makubaliano kuhusiana na bidhaa zilizothibitishwa ubora wake ambapo makubaliano hayo yanawezesha kila mzalishaji wa bidhaa aliyethibitisha ubora wa bidhaa yake kupeleka bidhaa hizo katika nchi yoyote Afrika Mashariki bila kukumbana na vikwazo ama wasiwasi juu ya ubora wa bidhaa husika na hivyo kuweza kushindana katika soko hilo,” alifafanua Haule.

Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, Haule alisema Serikali imetenga fungu maalum kwa ajili ya kuwawezesha kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, hivyo watapatiwa huduma hiyo bila gharama yoyote kwa muda wa miaka mitatu.

“Huduma ya uthibitishaji ubora wa bidhaa kwa wajasiriamali wadogo ni bure kabisa, kinachotakiwa ni wajasiriamali kupata barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na kuipeleka TBS, ambapo mchakato wa kuwapatia alama ya ubora unaanza mara moja,” alisisitiza.

Haule alisema TBS inatambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi wengi, ndiyo maana kuna mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali kwa kuwa na hilo ni sehemu ya majukumu ya shirika ili waweze kupata alama ya ubora.

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi wa TBS, Donald Mkonyi alitoa wito kwa wafanyabiashara wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi kusajili bidhaa na majengo yao.

“Natoa mwito kwa wafanyabiashara wote wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi kusajili bidhaa na majengo hayo ili kumhakikishia mtumiaji na mlaji usalama wake na kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza kwa watumiaji hao ama kero anayoweza kupata mfanyabiashara wakati wa zoezi la ukaguzi sokoni,” alisisitiza Mkonyi.

Mkonyi alielezea kuwa huduma zote za usajili na uthibitishaji ubora wa bidhaa kwa sasa zimerahisishwa zaidi na zinafanyika kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya TBS sehemu za mifumo ambapo wadau wote wanaweza kuleta maombi yao wakiwa mahali popote pale na yatashugulikiwa kwa wakati.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages