DC MBONEKO AAHIDI KUFUFUA SOKO LA DIDIA LILILOKIMBIWA NA WAFANYA BIASHARA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, September 5, 2021

DC MBONEKO AAHIDI KUFUFUA SOKO LA DIDIA LILILOKIMBIWA NA WAFANYA BIASHARAMkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiwa katika Soko la Didia wilayani Shinyanga ,ambalo limetelekezwa na Wafanyabiashara.

Na Marco Maduhu, Shinyanga

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, ameahidi kulifufua Soko la Didia wilayani Shinyanga, ambalo limetelekezwa na Wafanyabiashara kwa madai ya kukosa wateja.

Mboneko alibainisha hayo juzi alipotembelea Soko hilo, na kupewa taarifa kuwa, Wafanyabiashara wamegoma kulitumia kwa madai hawapati wateja, na hivyo kuamua kurudi kuuza bidhaa zao kwenye maeneo ambayo siyo rasmi.

Alisema kabla ya kurudisha wafanyabiashara kulitumia soko hilo, wataboresha kwanza miundombinu ya barabara, ili iwe rahisi wateja wawe kufika sokoni hapo, pamoja na kuhakikisha huduma za choo zinakuwa bora zaidi, ikiwamo upatikanaji wa maji ya kutosha.

“Naahidi kulifufua soko hili, ambapo pia tutawaondoa wafanyabiashara wa gulio ambao wamekuwa wakifanya shughuli zao kwenye Reli, waje kwenye soko hili ambapo kuna eneo kubwa tu hekari 10, eneo ambalo ni salama kwao na watachangamsha soko,”alisema Mboneko.

Awali Mtendaji wa kijiji cha Didia wilayani Shinyanga Masano Kwiyela, akitoa taarifa ya Soko hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, alisema lilijengwa mwaka 2012 kwa gharama ya Sh.milioni 107, lakini Wafanyabiashara wamegoma kulitumia kwa madai ya kukosa wateja.

Alisema walishawapatia vibanda bure Wafanyabiashara hao ili wauze bidhaa zao lakini hawakuchukua muda wakaondoka wote wakidai kuwa hawapati wateja na hivyo kulifanya soko kubaki tupu.

Nao baadhi ya Wafanyabiashara walisema, wameshindwa kufanya biashara kwenye Soko hilo, wakidai lipo mbali na muingiliano wa watu wengi (Center), ambapo wateja wamekuwa hawafiki huko, na kusababisha bidhaa zao kudolola.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akiwa katika Soko la Didia wilayani Shinyanga ,ambalo limetelekezwa na Wafanyabiashara.

Mtendaji wa kijiji cha Didia wilayani Shinyanga Masano Kwiyela, akitoa taarifa ya Soko la Didia kwa niaba ya Mtendaji wa Kata.

Muonekano wa ndani wa Soko la Didia.

Muonekano wa Nje wa Soko la Didia.

Na Marco Maduhu- Shinyanga


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

No comments:

Post a Comment

Pages