MWILI WA MZEE WA MIAKA 89 WAZIKWA BAADA YA KUKAA MOCHWARI MIEZI 8 RORYA | MALUNDE 1 BLOG

Saturday, September 4, 2021

MWILI WA MZEE WA MIAKA 89 WAZIKWA BAADA YA KUKAA MOCHWARI MIEZI 8 RORYA

  Malunde       Saturday, September 4, 2021

Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Wilson Ogeta

Hatimaye Familia ya Mzee Wilson Ogeta (89) wakazi wa Kijiji cha Nyambogo, wilayani Rorya mkoani Mara imeamua kuuzika mwili wa ndugu yao huyo aliyefariki dunia Januari 10, mwaka huu mara baada ya kukaa mochwari kwa muda wa miezi 8 baada ya familia hiyo hapo awali kugoma kuuzika kutokana na mgogoro wa ardhi.

Mwili wa Mzee Ogeta umehifadhiwa kwa zaidi ya siku 230 katika Hospitali ya Wilaya ya Utegi wilayani Rorya kutokana na kuibuka kwa mgogoro wa ardhi baina ya familia hiyo na mtu anayetajwa kununua ardhi ya mzee huyo

Wakizungumza na waandishi wa habari familia ya marehemu wameiomba serikali kuangalia namna ya kurejeshewa eneo lao ambalo lilichukuliwa kinyume na utaratibu.

Msemaji wa familia hiyo Isaya Goro alidai kuwa mzee huyo alianza kuugua mwaka 2016 na kupatiwa matibabu kwenye hospitali mbalimbali na Januari 10, mwaka huu alifariki dunia.

Alidai kuwa baada ya kufariki taratibu za msiba zilindelea kama kawaida na kupanga kumzika kwenye mji wake uliopo kijijini hapo, lakini wakiwa katika harakati za maandalizi ya mazishi Januari 15,2021 walipokea hati ya zuio la mahakama likiwataka kusitisha shughuli zote za maziko.

“Tukiwa tunajiandaa kuchimba kaburi hapa nyumbani tulipata stop order (zuio la mahakama) tukitakiwa kutofanya kitu chochote katika ardhi hii kwa madai kuwa ni mali ya mtu mwingine na si ya marehemu,” alidai.

Alisema kuwa baada ya kupata zuio hilo familia iliamua kwenda mahakamani kwa nia ya kutengua zuio hilo ili waweze kuendelea na mazishi, lakini uamuzi ukawa tofauti, kwani walishindwana wakaamua kwenda kuuhifadhi mwili wa marehemu katika Hospitali ya Utegi wakati wakiendeleza mapambano ya kudai haki.

Familia hiyo ilikata rufaa kupinga uamuzi huo wa mahakama ya wilaya ambapo rufaa hiyo ilianza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Julai 18, mwaka huu na kutolewa hukumu Julai 22 ambayo pia ilimpa ushindi mnunuzi wa eneo.

Baada ya hukumu hiyo familia haikuwa na namna ya kufanya isipokuwa kuacha mwili kuendelea kuwepo mochwari, huku wakiangalia namna ya kufanya kwa kuwa hawakuwa wametenga eneo lingine kwa ajili ya mazishi.

Alisema mgogoro huo umewaathiri kisaikolojia, kiuchumi na kuwazidishia machungu yasiyokwisha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambogo, Johannes Charles alisema kwa uelewa wake eneo hilo ni mali ya marehemu Ogeta na amekuwa akilitumia kwa miaka mingi na suala la uuzaji wa ardhi Serikali ya Kijiji ingeshirikishwa kila hatua.

Baadhi ya majirani walisema kuwa walishangazwa na taarifa za kuwa eneo hilo linamilikiwa na mtu mwingine tofauti na mzee Ogeta, ambaye amekaa katika eneo hilo miaka yote ya uhai wake hivyo kuomba uchunguzi wa kina ufanyike.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka ambaye alishiriki mazishi hayo alisema baada ya kupata taarifa za mgogoro huo aliwaita ndugu wa marehemu na mnunuzi na kuzungumza nao na kukubaliana kutafuta eneo lingine ambalo familia itaona linafaa kwa ajili ya mazishi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka, alishiriki katika mazishi hayo amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipinid hiki na wakati serikali ikishughulikia jambo hilo
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post