WAZIRI GWAJIMA: MSIWE WACHOYO WA UJUZI

Na WAMJW-DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wahitimu wa mafunzo ya muda mfupi ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko kuacha tabia ya kukaa na ujuzi walioupata badala yake wanatakiwa kuwafundisha na wenzao ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu.

Waziri Gwajima amesema hayo jana wakati aliposhiriki katika Mahafali ya 14 ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kilichoko jijini Dae Es Salaam.

“Nitoe rai kwenu wahitimu, msiwe wachoyo wa ujuzi mlioupata kupitia mafunzo haya na mtakaporudi kwenye vituo vyenu vya kazi mkabadilishane ujuzi na watumishi wenzenu ambao hawakubahatika kuhudhuria mafunzo haya”. Amesema Dkt. Gwajima.

Waziri Gwajima ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo itaboresha zaidi utendaji wa afua mbalimbali za ufuatiliaji, utambuzi wa haraka na udhibiti wa magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

“Hakikisheni mnakua chachu ya mabadiliko kiutendaji ili kuleta ufanisi na kuboresha ubora wa kazi zenu katika maeneo yenu ya kazi”. Ameongeza Dkt. Gwajima.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji ya afya ya jamii kwa kuboresha uwezo na kupunguza upungufu wa wataalam wa Epidemiolojia na udhibiti wa magonjwa nchini.

Mafunzo hayo ya awali yanakusudia kutoa wataalam wa epidemiolojia katika afya ya binadamu na Wanyama ilikuongeza ufanisi wa kufanya ufuatiliaji wa afya katika ngazi ya jamii na kuweza kutambua magonjwa ya milipuko na matukio mengine yenye athari kiafya kwa haraka, kuyatolea taarifa na kudhibitiwa kabla hayasababisha athari.

Mafunzo hayo yamekua yakitolewa kwa watumishi wa afya ya binadamu na mifugo chini ya ufadhili wa Shirika la kuzuia na kupunguza matishio ya magonjwa nchini Marekani la DTRA ambalo limekua likitoa msaada kwa awamu tofauti ambapo mahafali haya yanakua ya 14 na ya mwisho ambapo watumishi 41 wamehitimu kutoka Halmashauri 19 ya Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa na kufanya jumla ya watumishi 512 kuhitimu kutoka mikoa 26 na halmashauri 169 nchi nzima katika kipindi cha miaka 6.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments