DC KISWAGA : WATAKAOTOROSHA DHAHABU TUTAWASHTAKI KWA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kahama imemwagiza Kaimu Afisa Madini Kahama Jeremia Hango kufanya ukaguzi wa vitabu vya kumbukumbu za utunzaji wa taarifa za madini katika mialo yote inayohusika na uchenjuaji wa madini ya dhahabu baada ya kubaini uwepo wa vitendo vya udanganyifu na utoroshaji wa madini.

Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika machimbo ya Mwime gold mine na Bumbiti gold rush na kubaini udanganyifu huo unaotekelezwa na baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara ambao sio waadilifu.

Amesema kamati yake imefanikiwa kuwakamata wamiliki wa mialo 10 ambao hawatumii vitabu vya kutunza kumbumbu za madini hali ambayo inachangia dhahabu kutoroshwa na kuuzwa kwa magendo hali ambayo inachangia kuhujumu mapato ya serikali.

“Nimeagiza watozwe faini kwa mujibu wa sheria za madini na watakaobainika kukiuka sheria kwa makusudi hatutatoa nafasi ya kulipa faini na badala yake tutawapeleka mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi,hivyo nitoe rai kwa wachimbaji na wamiliki wa mialo kutojihusisha na vitendo hivyo,”amesema Kiswaga.

Amefafanua kuwa wezi na watoroshaji wa madini kahama hawana nafasi, kutokana na serikali kuweka mitego kila sehemu,atakayekamatwa atawajibishwa kwa makosa ya uhujumu uchumi,na kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara kuyatumia masoko halali yaliyotengwa na serikali kwaajili ya biashara ya madini.

“Ukiangalia hali ya uuzaji wa madini kwenye masoko yetu imeshuka lakini uzalishaji bado upo juu mwezi uliopita masoko yetu yaliuza dhahabu yenye kilogramu 25 ambayo imedhalishwa na wachimbaji wadogo lakini kwa sasa wameanza kutumia njia zisizo rasmi kutorosha madini tena,”amesema Kiswaga.

Sambamba na hilo Kiswaga amewataka wamiliki wa leseni ambazo hawaziendeleza kuhakikisha zinafanya kazi ili kupunguza malalamiko ya watu kukosa maeneo ya uchimbaji ilihali kunawatu wamehodhi leseni na wamekaa tu kinyume na maelekezo ya serikali.

Kwa upande wake Kaimu afisa madini mkoa huo Jeremia Hango amesema kuwa watatekeleza agizo hilo na kutoa rai kwa wamiliki wa mialo kizingatia maelekezo ya serikali ili kuepuka mkono wa sheria dhidi ya vitendo vya wizi wa madini.

“Tumetoa vitabu maalumu vya kutunza kumbumkumbu za taarifa za uzalishaji kwenye mialo hadi inaposafirishwa kwenda kwenye masoko lakini baadhi yao wanajaza taarifa za uongo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na tutakaowabaini tutawawajibisha,”amesema Hango.

Naye Mwenyekiti wa wachimbaji wa madini ya dhahabu wilaya ya Kahama Joseph Nalimi ameiomba serikali kuwapatia vifaa na elimu ya utambuzi wa miamba ili kuepuka uchimbaji wa kuhamahama ambao unachangia kuharibu mazingira.

“Serikali itupatie wataalamu wa miamba watakaotusaidia sisi kujua maeneo yenye madini ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuepuka hasara inayoweza kujitokeza pindi tunapowekeza katika maeneo ambayo hayana madini,”alisema Nalimi.
Mkuu wa wila ya kahama Festo Kiswaga akizungumza na wachimbaji hawapo pichani katika machimbo ya mwime gold mine.
Baadhi ya wachimbaji wa madini wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga.
Monica Charles akisambaza mchanga wenye madini ya dhahabau katika machimbo ya Bumbiti gold rush

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments