WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA POLE KWA FAMILIA YA KWANDIKWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa kimeacha pengo serikalini na Bungeni kwani marehemu alikuwa mchapakazi, mwadilifu na mtulivu katika utendaji kazi wake

Amesema hayo jana Jumatano (Agosti 4, 2021) alipokwenda nyumbani kwa marehemu Kwandikwa, Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani kutoa pole kwa familia.

“Mchango wake wa utendaji katika serikali  na Bunge ni mkubwa sana alifanikiwa kuwavutia wengi kwa tabia yake ya upole, unyenyekevu na uzingatiaji wa taratibu na sheria za utumishi  kila alipopangiwa kufanya kazi hivyo kifo chake ni pigo kwa taifa”

Mheshimiwa Majaliwa ameishukuru familia kwa kuridhia maombi ya kutaka mazishi yafanyike Jumatatu ijayo ili kuwapa nafasi waombolezaji wakiwemo wabunge kupata nafasi ya kusafiri kutoka waliko na kushiriki katika kutoa heshima za mwisho na mazishi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu leo  amekwenda nyumbani  kwa marehemu Biswad Msuya, Kaka Mkubwa wa Mkurugenzi Mkuu wa  Usalama wa Taifa kutoa pole kwa familia kufuatia kifo cha mpendwa wao.

Akizungumza na wafiwa na waombolezaji katika msiba huo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amepokea taarifa ya kifo cha marehemu Biswad  kwa mshtuko mkubwa na amewataka waombolezeji wamuombee mke wa marehemu na familia ili awape utulivu na uvumilivu wakati huu wa majonzi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments