SERIKALI YAMUAGIZA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA KUACHA MARA MOJA ZOEZI LA KUKAMATA DENGU..MAGARI YAACHIWE .. "KITENDO KILIICHOFANYIKA NI UBABE". '


Na Ramadhan Hassan,Dodoma

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema Mkoa wa Shinyanga unaenda kinyume na maelekezo ya wizara yake kukamata magari yanayobeba mazao ya dengu ,kunde na mbaazi hivyo amemtaka Mkuu wa Mkoa huo,Dk. Philemon Sengati kuacha zoezi hilo mara moja na kurudisha mazao aliyokamata kwa wenyewe.

Hatua hiyo imetokana na zaidi ya magari 30 yaliyokuwa yamebeba zao la dengu kuzuiliwa mkoani humo kwa madai ya kukiuka masharti ya stakabadhi ghalani.

Bashe ametoa maagizo hayo leo Agosti 27,2021, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuanzia sasa magari yote yaliyokamatwa katika mkoa wa Shinyanga yaachiwe mara moja.

Amesema kitendo hicho kinachofanywa na uongozi wa mkoa wa Shinyanga ni cha kibabe.

Amesema kuwa wafanyabiashara wana leseni lakini wanapofika katika Shinyanga wanakamatwa wakati mwenye mamlaka ya kuagiza zao liuzwe kwa namna gani katika minada ni waziri wa kilimo pekee.

“Jambo hili haliwezekani,wafanyabiashara wamelipa ushuru lakini wanakamatwa,hatutaki namna hii jambo hili sio zuri,”amesema.

Hata hivyo ,Bashe amesema hali hiyo haitajirudia Shinyanga huku akiwapa pole wakulima pamoja na wafanyabiashara waliopata kadhia hiyo.

“Niwahakikishie wakulima na wafanyabiashara wa nchi hii wizara ya kilimo itaendeelea kuwalinda kwa nguvu zote kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanakuwa rafiki,”amesema Bashe.

CHANZO - TIMES MAJIRA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments