PAROKO MAKANDAGU AWACHANA WANASIASA KWENYE MAZISHI YA NKULILA ....."WANASIASA NI WANAFIKI...PENDANENI"


Paroko wa Parokia ya Ngokolo Padre Adolf Makandagu akitoa mahubiri katika Misa ya kuombea mwili wa marehemu David Nkulila katika Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Ngokolo Mjini Shinyanga.Picha na Kadama Malunde

Na Marco Maduhu, Shinyanga
Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila (57) na Diwani wa Kata ya Ndembezi, aliyefariki dunia Agosti 23 mwaka huu, kwa matatizo ya ugonjwa wa Moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga, amezikwa leo Agosti 23,2021 kwenye Makaburi ya Mageuzi Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Awali akitoa Mahubiri kwenye Misa ya kuuombea Mwili wa Marehemu David Nkulila, kwenye Kanisa la Katoliki la Mama Mwenye Huruma Ngokolo , Paroko wa Parokia ya Ngokolo Aldof Makandagu, amewataka wanafamilia ya marehemu, wamtumainie Mungu na kuacha kusikiliza maneno ya walimwengu juu ya kifo cha mpendwa wao.

Amesema kifo cha Nkulila ni mapenzi ya mwenyezi Mungu ambapo muda wake umefika wa bwana kumtwaa, na kuwataka wanafamilia wazidi kuimarika katika imani.

“Naombeni wanasiasa mumuenzi Marehemu David Nkulila kwa vitendo, kwa kuguswa na matatizo ya watu, kuwatembelea kusikiliza kero zao na kuzitatua,”amesema Paroko Makandagu.

Katika hatua nyingine amewataka wanasiasa kupendana, na kuacha kuishi kwa unafiki na kupendana kwenye majukwaa tu, lakini wakitoka hapo hakuna upendo wa kweli na kuanza kusemana maneno mabaya usiku na mchana.

“Wanasiasa ni wanafiki hamna upendo wa kweli, mnapendana siku za kampeni na kwenye majukwaa, lakini mkitoka hapo hakuna kitu, na mnauana kwa maneno usiku na mchana na njia nyingine zisizo eleweka, ila simaanishi kwamba Nkulila ameuawa, ila pendaneni wanasiasa,”ameongeza.

Aidha, amesema kuna baadhi ya wanasiasa kwenye msiba huo wa Nkulila sura zao zinaonyesha zina huzuni, lakini Moyoni wanachekelea.

Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, akitoa neno kwenye Misa hiyo ya kumuombea Marehemu, iliyoongozwa na Padre Deusdedith Kisumo, ameitaka Serikali kuendeleza maono ya Marehemu Nkulila, kuufanya mji wa Shinyanga kuwa Jiji na kukamilisha mradi wa Machinjio ya kisasa.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Donald Magesa, amesema msiba wa Nkulila ni pigo kwa chama hicho, ambapo alikuwa mzalendo mtetezi wa wanyonge na mpenda maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, amesema Serikali imepoteza mtu muhimu sana, mwenye maono, mzalendo, na mjenga hoja, na mcha Mungu, huku akiahidi kumuenzi kwa kutekeleza maono yake yote ikiwemo Manispaa Shinyanga kuwa na hadhi ya Jiji na miradi ya maendeleo ili ambayo ameiacha.

Aidha, Diwani wa Lubaga Reuben Dotto, akisoma wasifu wa marehemu, alisema David Nkulila alizaliwa mwaka 1964 na amefanya shughuli mbalimbali kikiwemo Kilimo, ambapo mwaka 1987 ndipo akaingia kwenye siasa na ameshika nafasi mbalimbali za Uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dotto aliongeza kuwa, mwaka 2010 aliingia kwenye kugombea udiwani Kata ya Ndembezi kupitia CCM na mwaka 2013 alichaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga hadi 2015, na uchaguzi mkuu 2020 alishinda kiti hicho pamoja na kuwa Meya kamili hadi umauti unamfika Agosti 23 mwaka huu.

Msiba huo umehudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, Mbunge wa Msalala Iddi Kasimu, na Mbunge wa Viti maalumu Christina Mzava pamoja na viongozi wa Serikali na siasa na wananchi mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga.
 
Soma pia 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments