Picha & Video : WAFANYAKAZI WA TANESCO WAZUA GUMZO WAKIFYEKA SHAMBA LA MAHINDI TINDE


Leo Alhamis Agosti 19,2021 kuna video imesambaa mtandaoni ikiwaonesha wafanyakazi wa TANESCO wakikata mahindi yaliyolimwa na mwananchi aliyejulikana kwa jina la Hemed Rashid katika eneo la Tinde wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

Inaelezwa kuwa mahindi hayo yamelimwa kwenye njia kuu ya umeme.
Kwa mujibu wa mmiliki wa shamba hilo lililofyekwa mazao yake, Hemed Rashid amesema aliamua kulima mazao hayo yakiwemo Mahindi, nyanya, mbogamboga na matikiti kufuatia kile alichosema ni Tamko la aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli kuruhusu wananchi walime mazao katika eneo hilo alipopita Tinde akitokea Chato Januari 29,2021 baada ya mmoja wa wananchi kutoa kero ya wananchi kuharibiwa mazao yao na TANESCO kila wanapolima.

"Rais aliruhusu wananchi tulime mazao yasiyoathiri nyaya za umeme wa TANESCO,akatoa angalizo tusipande miti wala kujenga nyumba, ndivyo tulivyofanya, sasa tumelima bahati mbaya hawa TANESCO hata ile kutoa tu taarifa kwamba tusilime haikuwepo, sasa mimi umekuta mazao yapo shambani kwanini usinishitaki tu mahakamani badala ya kuharibu mazao yangu ukaacha mahindi hayo kama yalivyo..Mahakama ndiyo itaamua kama mimi nina makosa au la.",amesema Hemed akizungumza na Malunde 1 blog.

“Mimi nimelima mazao hayo kwa jeuri ya Tamko la Rais ina maana ni sharia tosha,haihitaji tena mjadala, Rais akishasema hivi inabidi umfuate na hakuna tamko lolote lililotolewa kutengua tamko la Rais, wao wamekuja tu kufyeka mazao, wameng’oa nyanya, matikiti, vitunguu, mahindi na mbogamboga ambavyo nilikuwa nalima kwa njia ya umwagiliaji”,ameongeza Hemed.

Kufuatia tukio hilo Hemed amesema amepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 5.

Wakazi wa Tinde na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanahoji :
"Hii ni halali ? Kwanini tunarudishana nyuma namna hii? Hii Tinde pata picha huyu mkulima  amelima TANESCO wakiwa wamemtazama Ila leo wameamua kuja kukata mimea hivi mnadhani mwananchi atawaelewaje? Haya mahindi yana athiri nini kwenye nguzo ? Kuna mimea ya tikiti nayo imekatwa madhara ya hiyo mimea 362 ya tikiti ni yapi?".

"Tunaomba mamlaka kutusaidia kwani kitendo hiki ni ukatili dhidi ya binadamu maswali hayana majibu, Je shamba hili lilimwa siku moja na kupandwa kisha mazao kukua kwa kasi? Je Mamlaka ya Tanesco haikuwahi kufika hapo tangu shamba linalimwa hadi mazao yalipochanua kiasi hicho ndipo wakayaona?

 Na je kwa  kwa kuwa yalikuwa yamelimwa na kuchanua kiasi hicho kile kinachoitwa taratibu  zingine ukiacha Sheria na kanuni zilishindwa kufanyika na kuonya? au yalikuwa maksudi ya kufanywa  ukatili huo ndiyo maana mahindi yakaachwa yapendeze ndipo yafyekwe? Bado tunajiuliza tukisubiri taarifa za kimamlaka", wameendelea kuhoji watumiaji wa mitandao ya kijamii walioona video clip hiyo.

 
Soma pia:

Tazama picha na video zikionesha mimea hiyo ikikatwa
Mahindi yakikatwa
Mahindi yakikatwa
Miche ya matikiti ikiondolewa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments