BARRICK KUFANIKISHA KANUNI YA USHIRIKISHWAJI WATANZANIA KATIKA MNYORORO WA UCHUMI WA MADINI KWA VITENDO - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, August 1, 2021

BARRICK KUFANIKISHA KANUNI YA USHIRIKISHWAJI WATANZANIA KATIKA MNYORORO WA UCHUMI WA MADINI KWA VITENDO

Mwenyekiti wa Tume ya Madini,Profesa Idris Kikula (Kushoto) akibadilishana mawazo na Meneja wa Barrick nchini,Georgia Mutagahywa (Kulia) na Kamishna wa Madini kutoka Tume ya Madini,Janeth Lekashingo wakati wa warsha hiyo.
 ***
Kampuni ya madini ya Barrick, imeeleza dhamira yake ya kujipanga zaidi kuhakikisha inafanikisha kutekeleza kwa vitendo kanuni ya Serikali inayoyataka makampuni ya madini kushirikisha Watanzania katika mnyororo wa uchumi wa madini.

Haya yamebainishwa katika warsha ya siku mbili kuhusiana na utekelezaji wa kanuni hiyo, iliyoandaliwaTwiga Minerals Corporation na Barrick na kuhudhuriwa na Mameneja Waandamizi wa kampuni hizo, Mwenyekiti na watendaji waandamizi wa Tume ya Madini , wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali iliyofanyika katika mgodi wa Barrick North Mara.

Akitoa mada kuhusu jitihada zinazofanywa na Barrick kutekeleza kanuni hiyo, Meneja wa barrick nchini, Georgia Mutagahywa, alisema kampuni imeanza kutekeleza kanuni kwa vitendo katika maeneo ya ajira, utoaji wa zabuni, sambamba na kuendesha miradi ya kusaidia jamii katika maeneo yanazozunguka migodi yake ya Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara, kupitia sera ya kampuni ya kuhudumia jamii (CSR).

Miradi inayotekelezwa na Barrick imelenga kuboresha miundo mbinu mashuleni na vituo vya afya ,kuwapatia wananchi elimu ya ujasiriamali, maji safi na miundo mbinu ya barabara .

Hata hivyo alisema kampuni inahitaji ushirikiano zaidi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali inazokumbana nazo katika utekelezaji wa Sheria ya Madini na kanuni hii.

Mutagahywa, alisema kampuni iko mbioni kuanzisha programu ya kuendeleza biashara za wananchi (Local Business Development Programme (LBD), ambayo itakuwa kitovu cha kusimamia kanuni hii na kuhakikisha watanzania wananufaika nayo kwa asilimia kubwa kwa kuboresha maisha yao kupitia uwekezaji katika sekta ya madini,

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha hii, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa.Idrisa Kikula, alisema kuwa tangia tume hiyo ianze kufanya kazi, imekuwa mstari wa mbele kuratibu ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini.”Tumekuwa tukifuatilia kuhakikisha watanzania na makampuni ya wazawa yanapewa kipaumbele katika zabuni za kuuza bidhaa na kutoa huduma kwenye migodi isipokuwa huduma ambazo hazipatikani na ufuatiliaji huu umeanza kuleta matokeo mazuri”alisema.

Profesa Kikula, aliendelea kueleza kuwa tume ya madini iko tayari kusaidia Twiga kuhakikisha inafanikiwa kutekeleza kanuni hii inayotoa fursa kwa watanzania kunufaika na ushirikishwaji katika mnyororo wa uchumi wa madini kwa kutoa ufafanuzi wa changamoto mbalimbali ambazo kampuni inapambana nazo katika utekelezaji wake.

Warsha hii iliendeshwa kwa njia ya majadiliano na mafunzo ambapo wataalamu wa uendeshaji shughuli za madini kutoka Tume ya Madini, Janeth Lekashingo, Terrence Ngole na Godfrey Nsemwa, walitoa mada mbalimbali zinazoelekeza na kufundisha ufanikishaji wa utekelezaji wa kanuni hii.

Kanuni ya ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa uchumi wa madini, inaelekeza wawekezaji katika sekta hii kuweka kipaumbele katika matumizi ya bidhaa na huduma zinazozallishwa nchini isipokuwa bidhaa zinazohitajika ambazo hazipatikani nchini ambapo wazabuni wanaotumika kuagiza bidhaa hizo wanapaswa kushirikiana na makampuni ya wazawa, hali ambayo itakuza sekta ya biashara nchini na hivyo kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,Kanuni hii pia inaelekeza kutoa ajira kwa watanzania na kuondoa tofauti ya mishahara kwa wanaofanya kazi zinazofanana
Washiriki wa warsha hiyo wakifuatilia mada mbalimbali


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages