SERIKALI YA TANZANIA KUTENGENEZA CHANJO YA CORONA


Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 kwenye shule na Taasisi za Vyuo zinazotarajiwa kufunguliwa hapo kesho.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Prof. Carolyne Nombo akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo wakati wa kutoa tamko la Serikali kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 kwenye shule na Taasisi za Vyuo zinazotarajiwa kufunguliwa hapo kesho

**


Na Mwandishi wetu Dodoma

Serikali imeanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya Virusi vya Corona hapa nchini ili kupunguza gharama ya kuagiza nje ya nchi na kuzifanya ziwe karibu na wananchi.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dodoma Katibu Mkuu, Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Afya Prof. Abel Makubi amesema kiwanda hicho hakitatengeneza chanjo ya UVIKO tu bali na magonjwa mengine.

"Wataalamu tunao wengi na kiwanda hicho hakitatengeneza chanjo ya UVIKO 19 pekee, hata ikiisha tutaendelea kuzalisha chanjo nchini", alisema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesema Serikali haina mpango wa kuwauzia wananchi chanjo ya ugonjwa UVIKO 19 wala kuruhusu mtu yeyote kuingiza chanjo hiyo kinyume na utaratibu utakaowekwa.

Wakati huo huo, Prof. Makubi aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewataka viongozi na wasimamizi wa shule kuzingatia mwongozo wa kudhibiti ugonjwa wa UVIKO 19 ili kujikinga bila kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.

Amesema wakati shule na baadhi ya taasisi za vyuo zinatarajiwa kufunguliwa hapo kesho, mwongozo utakaotumika ni ule ule uliotumika mwaka jana na umepitiwa upya ili kuendana na mahitaji ya sasa

Prof. Makubi amesema Serikali inalazimika kuwakumbusha viongozi wa shule na Taasisi za Elimu kuimarisha mifumo ya malezi kwenye mabweni, kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara kuhusu afya za wanafunzi.

"Mambo muhimu ni viongozi wa shule na vyuo kuandaa miundombinu ya maji na upatikanaji wa barakoa kama ilivyokuwa mwaka jana na kuchukua hatua stahiki iwapo kutagundulika kuna maambukizi bila hofu wala taharuki" alisisitiza Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesisitiza elimu ya kujikinga na ugonjwa huo iendelee kutolewa kwenye maeneo mbalimbali hasa nyumba za ibada, shuleni na vyuoni.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Elimu Prof. Carolyne amesema Wizara kwa kushirikiana na Tamisemi itasimamia miongozo hiyo iliyotolewa na Wizara ya Afya.

"Miundombinu yote ifufuliwe ikiwemo matumizi ya vitakasa mikono, barakoa asilia na maji yanayotiririka" amesisitiza Prof. Carolyne.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments