WAAJIRI NA MAMLAKA ZA NIDHAMU TEKELEZENI MAAGIZO YA TUME YA UTUMISHI WA UMMA | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, June 22, 2021

WAAJIRI NA MAMLAKA ZA NIDHAMU TEKELEZENI MAAGIZO YA TUME YA UTUMISHI WA UMMA

  Malunde       Tuesday, June 22, 2021

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, jaji (mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana (aliyekaa katikati) akisaini nyaraka wakati wa Mkutano wa Tume Na. 4 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ulioanza leo Jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mheshimiwa George Yambesi , Kamishna wa Tume (kushoto) na Bw. Nyakimura Muhoji (kulia) Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma. (Picha na PSC)

***
Waaiiri na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma wamekumbushwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma kwa wakati na kama hawaridhiki na uamuzi na maagizo ya Tume wanayo nafasi na haki ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven James Bwana amesema haya jana wakati wa Mkutano wa Tume Namba Nne wa mwaka wa fedha 2020/2021 unaofanyika Jijini Dar es Salaam. Katika Mkutano huu Tume itapokea na kutolea uamuzi Rufaa 107 na Malalamiko 06 yaliyowasilishwa na Watumishi mbalimbali wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka zao za Nidhamu.

“Tume imekuwa ikitoa maelekezo kwa Waajiri, Mamlaka za Nidhamu na Mamlaka nyingine lakini baadhi yao wamekuwa wanakataa kutekeleza maagizo ya Tume bila kuwa na sababu za msingi. Tume ya Utumishi wa Umma imekabidhiwa Mamlaka ya kuhakikisha kuwa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo. Kama hawaridhiki na uamuzi na maagizo ya Tume wanayo nafasi na haki ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais, ambaye uamuzi wake ni wa mwisho”,alisema Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana.

Akizungumza katika Mkutano huo, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) John Haule alisema bado kuna tatizo katika utekelezaji wa maagizo yanayotolewa na Tume, mathalani baadhi ya Waajiri kutochukua hatua kwa wakati. “Ni muhimu kuchukua hatua kwa kuzingatia Sheria zilizopo”, alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nyakimura Muhoji alisema Tume imekuwa ikizikumbusha mara kwa mara Mamlaka kuchukua hatua stahiki kama maelekezo ya Tume yanavyotolewa.

“Mamlaka zingine zimekuwa hazitekelezi maagizo yanayotolewa na Tume kwa wakati. Hali hii haiwezi kuendelea, ni lazima Tume itachukua hatua kwa Mamlaka ambazo zimekuwa hazitekelezi maagizo ya Tume”, alisema Muhoji.

Mkutano wa Nne wa Tume kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ulianza jana tarehe 21 Juni na unafanyika hadi tarehe 02 Julai 2021, Jijini Dar es Salaam.

Tume ya Utumishi wa Umma inatekeleza majukumu haya kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya mwaka 2019).


Imeandaliwa na:-

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Tume ya Utumishi wa Umma

DAR ES SALAAM

22 Juni, 2021
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post