JESHI LA POLISI SHINYANGA LAWAKAMATA WANAODAIWA KUMUUA HADIJA KISINZA

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia vijana wawili Shinje Ngula (23), Mkazi wa Mawemilu Wilaya ya Shinyanga na   Kisinza Lusamila (28) mkazi wa Mpanda mkoani Katavi kwa tuhuma ya mauaji ya Hadija Kisinza Holo  (60) mkazi wa Mawemilu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mjini Kahama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema inadaiwa kuwa tarehe 14/12/2020 majira ya saa 02:00 usiku katika kijiji cha Mawemilu Tarafa ya Nindo Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Mkoa wa Shinyanga  Hadija Kisina Holo akiwa ndani ya nyumba yake aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali  kichwani na watu wasiofahamika. 

"Mara baada ya tukio hili kutokea upelelezi ulifanyika na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa Shinje Ngula (23) na  Kisinza Lusamila (28) mnamo tarehe 19/05/2021 huko Mpanda Mkoani Katavi kufuatia msako mkali uliofanywa na kikosi kazi cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa",amesema Kamanda Magiligimba.

Ameeleza kuwa watuhumiwa wamekiri kuhusika na mauaji hayo na taratibu za upelelezi zinaendelea na zitakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa dhidi ya watuhumiwa wengine waliohusika kwenye tukio hilo la sivyo wajisalimishe wenyewe kwani watakamatwa tu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments