JAMAA ACHOMA MOTO GODORO NA NGUO ZA MAMA MKWE BAADA YA MKE WAKE KUMTOROKA

Maafisa wa polisi eneo la Kiminini kaunti ya Trans Nzoia nchini Kenya wanamsaka jamaa mmoja mwenye umri wa makamo aitwaye Amos Wanjala ambaye anadaiwa kuvamia makazi ya mamake mkwe na kuchoma malazi yake.

Inaelezwa kuwa Amos Wanjala alitekeleza kitendo hicho baada ya mkewe kumtoroka.

Akiwa mwenye ghadhabu, Wanjala alivamia boma la Mercyline Wanyama Alhamisi, Mei 28,2021 mwendo wa saa tano usiku, alimuasha mama mkwe na kisha kuchoma malazi na baadhi ya nguo zake.

Mama huyo alisema alipoteza mali inayogharimu zaidi ya KSh 6,000 kwenye mkasa huo na hadi kwa sasa anashangaa ni nini kilichomfanya mkwe wake kumvamia.

Mshukiwa anasemekana kumtishia maisha mama huyo, hii ni kulingana na OCPD wa Kiminini Francis Tumbo.

Tumbo alisema mshukiwa akikamatwa, atashtakiwa kwa uharibifu wa mali na pia kumtishia maisha mama huyo.

"Akishakamatwa, atashtakiwa kwa kosa la kuharibu mali," OCPD huyo alisema.

Kwa mujibu wa taarifa za The Standard, mkaaji mmoja aliyetambulika kama Juma Barasa ametaka mshukiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria kutokana na kukiuka mila.

"Ni kinyume na ukoo wa Wabukusu kwa mtu yeyote kuwashambulia wakwe zake ama kuharibu mali yao," Barasa alisema.

Mmoja wa majirani amesema kwamba Wanjala atapigwa faini ya mbuzi ambayo itachinjwa kwenye sherehe ya utakaso.

Chanzo - Tuko news

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments