WAFANYABIASHARA WADOGO MOROGORO WAPEWA MBINU ZA KUTIBU MAJI

 Wafanyabiashara wadogo katika soko la Mawenzi, soko la Madizini na soko la Mji Mpya yaliyopo katika manispaa ya mji wa Morogoro wamejengewa uwezo wa namna ya kutumia mbinu mbalimbali kutibu maji. Katika mafunzo hayo yaliyoendeshwa na shirika la Raleigh Tanzania.

Mafunzo hayo yamefanyika Ijumaa Aprili 10, 2020 ambapo wafanyabisahara walifundishwa kwa vitendo mbinu mbalimbali za kutibu maji kwa lengo la kuhakikisha wanadumisha usafi na usalama wa afya zao na wateja wao kwa kutumia maji safi na salama. 

Akizungumza baada ya zoezi hilo (mwakilishi wa Raleigh Tanzania, Bi. Jovina Justus alisema baadhi ya mbinu walizofundishwa wafanyabiashara hao ni pamoja na kutibu maji kwa njia ya vidonge, kutibu maji kwa kutumia mitungi maalumu ya kuchujua maji, kuchemsha na kuchuja. Jovina aliongeza kwamba mbinu hizo ambazo nyingi ni za asili zitawasaidia wafanyabiashara hao kudumisha usalama wa afya zao kwa kuhakikisha wanatumia maji safi na salama.

“Mbinu hizi ambazo nyingi ni za asili zitawasaidia wafanyabiashara wa eneo hili kukabiliana na changamoto ya matumizi ya maji yasiyo safi na salama. Kwa sasa wafanyabiashara wengi hasa wafanyabiashara wanaofanya biashara ya kuuza chakula wanafahamu umuhimu wa maji safi na salama lakini pia wanafahamu namna ya kutibu maji”, alisema Jovina Justus.

Kwa upande wa wafanyabisahara hao walizungumza namna walivyonufaika na mafunzo hayo na kuwashukuru waandaaji Raleigh Tanzania kwa kuwaletea jawabu la maji safi na salama. 

“Mwanzo sikutaka kushiriki katika mafunzo haya kwani niliona kama napoteza muda wangu lakini nimejikuta nimechota maarifa mengi sana kwa muda mfupi. Nilikuwa nikisikia tuu kuhusu maji safi na salama lakini sikuwahi kuchukua hatua yoyote, kwa sasa nafahamu hasa nini cha kufanya ili kutibu maji. Kuanzia sasa siwezi kutumia tena maji ambayo hayajitibiwa kwani hakuna gharama yoyote ya kutibu maji”, alinukuliwa Bw. Felix Mwingizi mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo. 

Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo aliwaomba waandaaji wa mafunzo hayo kufikisha mafunzo hayo kwa wananchi wengi zaidi ili kusaidia kukabiliana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyotibiwa.

“Mimi binafsi nimejifunza kwa vitendo namna ya kutibu maji, hii itanisaidia mimi na watu walionizunguka. Natamani mafunzo haya yangewafikia watu wengi zaidi hasa katika ngazi ya kaya ili kuzisaidia familia kujiepusha na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama”, alisema mshiriki huyo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya kampeni iliyopewa jina la Kijana Ni Usafi inayotekelezwa na shirika la Raleigh Tanzania kwa lengo la kuhimiza usafi binafsi na usafi wa mazingira kwa vijana. Kampeni hiyo inayotekelezwa na Shirika la Msaada la Uingereza (UKAID) inalenga wanawake na wanaume wenye umri wa miaka 15-35. Kampeni hiyo inatarajia kuwafikia vijana 48,000 katika mikoa minne ambayo ni Iringa, Dodoma, Dar es salaam na Morogoro.

Mkoani Morogoro, lengo kuu la kampeni ni kuhimiza matumizi ya maji salama katika jamii. Sababu kubwa ni kwamba mkoa wa Morogoro umeathiriwa na magonjwa kama vile homa ya matumbo, kuhara na mlipuko wa kipindupindu mara kwa mara. Wanajamii wanaathirika kutokana na tabia ya kutumia maji yasiyo salama.

 Kampeni imepewa jina la "Tumia Maji Salama, Okoa Mkwanja" kuonesha vijana namna ambavyo matumizi ya maji salama yatawaepusha na gharama za kutibu magonjwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments