SERIKALI YAAGIZA MAAFISA ELIMU KATA KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI YOTE YA ELIMU IKAMILIKE KWA WAKATI


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa David Silinde

Na Fred Alfred -Dodoma
SERIKALI imewaagiza maafisa elimu kata kuhakikisha wanasimamia fedha na miradi yote ya elimu katika shule za msingi na sekondari ili ikamilike kwa wakati na kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa jana jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa David Silinde wakati akifungua kikao cha maafisa elimu kata nchini(UMEKTA).
“Kuhusu usimamizi wa fedha na miradi ya elimu, kila Afisa elimu kata asimamie miradi na fedha zote za serikali ndani ya kata yake kwa shule zote za msingi na sekondari.

“Baadhi yenu mnazembea kwenye usimamizi na kuisababishia Serikali hasara na kutokuonekana kwa thamani ya fedha kwenye baadhi ya miradi inayotekelezwa katika Kata zetu,”alisema.

Silinde alisema imebainika kuwa baadhi ya walimu wamekuwa na mikopo mingi kupita kiasi inayopelekea kukosa utulivu kazini na kusababisha utendaji kazi usioridhishi hivyo kila Afisa Elimu kata ahakikshe kuwa, walimu wanaelimishwa juu ya madhara ya mikopo hiyo.

Alisisitiza liwa maafisa elimu kata wanatakiwa kusimamia kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika Shule za Msingi na Sekondari kwa kuwa imebainika kuwa baadhi ya Maafisa Elimu kata hawasimamii shule za Sekondari.

“Kila Afisa Elimu Kata afanye tathmini ya maendeleo ya taaluma kwenye kata yake ili kubaini changamoto zinazokwamisha utoaji wa elimu bora ndani ya kata husika na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikisha jamii na viongozi wa kata husika,”alieleza.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Gerald Mweli alisema Serikali imewawezesha maafisa elimu kata kwa kuwapa nyenzo ya usafiri pamoja na posho ya kuwasaidia kutekeleza majukumu yao.

Alisema hata hivyo, baadhi wamekuwa hawatimizi majukumu yeo ipasavyo ikiwemo kutokufika kwenye shule kwa muda mrefu.

“Tutakuwa na usimamizi wa karibu kuona kuwa, mnatekeleza majukumu yenu, na pale ambapo itabainika kuwa na udhaifu au uzembe, hatua kali za kisheria na kiutumishi zitachukuliwa dhidi ya wahusika,”alieleza.

Naibu katibu mkuu aliongeza kuwa ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwenye Shule za Msingi na Sekondari, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, Washirika wa Maendeleo na jamii imejenga vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na hivyo kuongezeka kutoka 115,665 mwaka 2015 hadi kufikia 136,292 mwaka 2020.

“Wakati huo huo, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020 na shule za Sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi 5,330 mwaka 2020,”alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments