RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KATIBU MTENDAJI WA SADC


Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax, ambaye amempa taarifa juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Jumuiya hiyo.

Wakati wa mazungumzo hayo Dkt. Tax amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushika madaraka ya Urais na kuwa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania na amempongeza kwa hotuba nzuri aliyoitoa Bungeni jana ambayo imetoa mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita.

Dkt. Tax ambaye anamaliza muda wake wa miaka 8 mwezi Agosti mwaka huu, ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano alioupata wakati wote akiwa Katibu Mtendaji wa SADC na ameipongeza Tanzania ambayo wakati wa uenyekiti wake wa SADC imeandaa na kukamilisha mkakati wa maendeleo wa SADC licha ya kuwepo kwa janga la corono.

Aidha, amesema katika kipindi hicho SADC imeendelea kuwa na utulivu wa kisiasa ambao umetoa fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi, hivyo ametoa wito kwa Tanzania kutilia mkazo katika uimarishaji wa sekta za uzalishaji kama vile viwanda, kilimo, biashara, kusimamia ubora na kuendeleza miundombinu.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Dkt. Tax kwa kuiwakilisha vizuri Tanzania katika utumishi wake akiwa Katibu Mtendaji wa SADC na ameahidi kufanyia kazi ushauri na fursa mbalimbali ambazo SADC anazitoa kwa Tanzania.

Rais Samia Suluhu Hassan amemkaribisha nyumbani baada ya kumaliza muda wake ili aungane na Watanzania katika ujenzi wa Taifa.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments