WANANCHI NYALIGONGO WAKABIDHI MSAADA WA MADAWATI SHULENI, DC MBONEKO AONYA WAZAZI KURUBUNI WATOTO KUFELI MTIHANI

 


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, kulia akipokea msaada wa Madawati, kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Nyaligogo Masumbuko Lushona kushoto, ili kupungufa upungufu wa madawati katika shule ya Msingi Nyaligongo wilayani Shinyanga.

Na Marco Maduhu, Shinyanga.

Wananchi wa kijiji cha Nyaligongo Kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga, wametoa msaada wa madawati 100 katika shule ya Msingi Nyaligongo, ili kumaliza tatizo la upungufu wa madawati shuleni hapo.

Msaada huo wa madawati umetolewa jana shuleni hapo, na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Shnyanga Jasinta Mboneko, ili kuboresha mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma na kutimiza ndoto zao.

Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Nyaligongo Masumbuko Lushona, amesema fedha za utengenezaji huo wa madawati zimechangwa na wananchi kwa lengo la kuondoa adha ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini, na sasa wapo kwenye ukamilishaji wa madawati mengine 100.

“Wananchi wa kijiji hiki cha Nyaligongo tunaungana na Serikali kuboresha miundombinu ya elimu, ili watoto wetu wasome katika mazingira mazuri na kupata ufaulu mzuri na kutimiza ndoto zao, na kuja kuwa msaada kwetu hapo baadae,”amesema Lushona.

Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Zephania Daudi anayesoma darasa la nne , amesema wanafunzi wanapokuwa wakisoma huku wamekaa chini, ufanisi wa kusoma hua ni mdogo huku wakikabiliwa na miandiko mibaya, lakini wakikaa juu ya madawati usomaji wake huwa ni tofauti pamoja na kuwa ni miandiko mizuri.

Naye Mwanafunzi Elizabeth Maduhu, amesema uwepo wa madawati ya kutosha shuleni, hata ufaulu wa wanafunzi utaongezeka pamoja na kupunguza utoro, sababu ya kuwapo na mazingira mazuri ya kujisomea na kutimiza ndoto zetu.

Aidha Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Emmanuel Raymond, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,300 na inakabiliwa na upungufu wa madawati 250.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amewapongeza wananchi hao kwa kuchangia madawati hayo, huku akiwataka wanafunzi wasichole chole madawati hayo pamoja na kupanda juu ili yasivunjike, bali yadumu kwa muda mrefu na kusoma katika mazingira mazuri.

Katika hatua nyingine Mboneko amewaonya wazazi na walezi, kuacha tabia ya kuwarubuni wanafunzi wa kike wafanye vibaya kwenye mitihani yao, ili wapate mwanya wa kuwaozesha ndoa za utotoni kwa tamaa ya kupata mali, bali wawaache watimize ndoto zao na kuja kuwasaidia hapo baadae.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kulia), akikabidhiwa madawati 100 na uongozi wa Serikali ya kijiji cha Nyaligongo kwa ajili ya kupunguza upungufu wa madawati katika shule ya msingi Nyaligongo, kushoto ni mwenyekiti wa kijiji cha Nyaligongo Masumbuko Lushona.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza na wanafunzi wa shule ya Msingi Nyaligongo wilayani Shinyanga na kuwataka wasiharibu madawati hayo, bali wasome kwa bidii na kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga akiendelea kuwapa nasaha wanafunzi wa shule ya Msingi Nyaligongo juu ya kupenda elimu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Nyaligongo Emmanuel Ryamond, akizungumza mara baada ya kupata msaada huo wa madawati.
Mwanafunzi wa shule ya Msingi Nyaligongo Elizabeth Maduhu, akielezea faida ya shule kuwa na madawati ya kutosha na kushukuru kupatiwa madawati hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akipiga picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Nyaligongo mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upokeaji wa madawati 100.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments