GEKUL AAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO KWA WADAU WA TASNIA YA HABARI NCHINI



Rais Samia Suluhu Hassan akimwapisha Pauline Gekul kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma jana.

Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (asiye na Miwani) akizungumza na Viongozi Wakuu wa Wizara; kushoto ni Naibu wake Mhe. Pauline Gekul, kulia ni Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas na wa kwanza ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ally Possi, mara baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma jana.Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ally Possi (katikati) na Mkurugezi wa Utawala wa Wizara hiyo Bernard Marcelline mara baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma jana.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas(mwenye suti ya bluu) na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ally Possi, mara baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma jana.


Na John Mapepele, Dodoma

 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Pauline Gekul ameahidi kuimarisha ushirikiano  kwa wadau wa  tasnia za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kutimiza  ahadi za Ilani ya Chama cha Mapinduzi  na  ahadi alizozitoa Mheshimiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan wakati wa Kampeni za Uchaguzi   Mkuu mwaka 2020. 

Mhe. Gekul ameyasema haya muda mfupi baada ya kuapishwa  kuwa Naibu Waziri kwenye tasnia hizo na Mhe. Rais kwenye Ikulu ya  Jijini Dodoma jana ambapo amewahakikishia wadau wote nchini kuendeleza ushirikiano  ili kuleta mapinduzi makubwa katika Wizara hiyo kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana hiyo Mhe. Innocent Bachungwa.

“ Nitatoa ushirikiano kwa Waziri wangu lakini pia kwa wadau wote wa tasnia hii ya Wizara yetu ili kuhakikisha michezo, utamaduni, habari, Sanaa kila jambo liende  kulingana na ahadi alizotoa  mama yetu mpendwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ” amesisitiza Gekul

Amesema katika kutenda kazi hii mpya pia atazingatia miongozo aliyoitoa Mhe. Rais kwenye hotuba yake awali ambapo alielekeza mambo mahususi ya kuyafanyia kazi.

Akizungumzia uteuzi wa Naibu Waziri Gekul mara baada ya kukamilisha zoezi la kuwaapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri na Manaibu Mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amesema. “Nimemtoa Wizara ya Mifugo, pengine anajua mambo ya mifugo mifugo, lakini nikaona aende kwenye michezo awasaidie wanawake”

Amesema wanawake wamefanikiwa kuleta vikombe vitatu hapa nchini na hawatajwi kama ilivyo kwa upande wa wanaume ambapo ameeleza kuwa awali yeye ndiye alipewa kazi hiyo kwenye kipindi cha kwanza cha Awamu ya Tano na Hayati, Rais Magufuli hivyo amempa  Mhe. Gekul kwa matarajio makubwa.

 

 Amefafanua kuwa wanawake wamekuwa akifanya vizuri kwenye michezo mbalimbali hivyo aende akasimamie hilo kikamilifu

“Wanawake kwenye michezo wanafanya vizuri, hawasifiwi lakini wanaume wakishinda tu, katia goli huku viwanja vinagawiwa” ameongeza Mhe. Rais Samia.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwa  na Imani nao na kuendelea kuwateua kusimamia tasnia hizo na kumuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano, uadilifu na ubunifu mkubwa  ili kutimiza ahadi za Serikali kwa wananchi wake.

“Kipekee ninamshukuru  sana Rais wangu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea  kutuamini naomba kumhakikishia kuwa tutafanya kazi  bila kuchoka  na kwa ushirikiano  mkubwa  baina yetu sote, sisi  na wadau wetu wote ili kukamilisha ahadi katika kipindi kifupi” ameongeza Mhe. Bashungwa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments