ONGEZEKO VIFURUSHI 'BANDO' KILIO KILA KONA... STEVE NYERERE ATAKA WAZIRI ASEME WALAU NENO MOJA TU


Kulia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Faustine Ndugulile, kushoto ni msanii wa filamu Steve Nyerere
**

Mapema leo Ijumaa Aprili 2, 2021 kumeibuka mjadala  mkubwa miongoni mwa watumiaji simu za mkononi baada ya mambo kuwa kinyume na matarajio yao licha ya kuanza kutumika kwa kanuni mpya za huduma leo.

Watumiaji mbalimbali wa Mitandao ya Kijamii kila kona wanaendelea kulalamikia kuhusu ongezeko la Vifurushi 'Bando' kwenye mitandao ya simu lililoanza leo Aprili 2,2021 nchini Tanzania.

Miongoni mwa waathirika wakubwa wa ongezeko la vifurushi ni waandishi wa habari ambao shughuli zao za kila siku zinahitaji huduma ya intaneti/vifurushi ili kufikisha habari kwa jamii.

Kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) zimeanza kutumika leo matumaini ya wengi ilikuwa ni bei za vifurushi kupungua lakini imekuwa tofauti.

Msanii wa filamu Steve Nyerere amemuomba Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Faustine Ndugulile kuingilia kati na kutoa japo neno moja kuhusu changamoto iliyokuwepo kwenye mitandao ya simu hasa upande wa vifurushi.

Kupitia ujumbe wa Steve Nyerere aliomuandikia Waziri huyo kupitia mtandao wa Instagram unaeleza kuwa:

"Mhe. Waziri nakuomba sema neno 1 tu kwenye suala la bando na vifurushi, hili ni janga na msiba wa wanyonge wanalia kila kona, najua unajua kwani Serikali haijawahi kushindwa kitu kwa kusimama na wananchi wao, ipo tija ya haraka sana kukaa kikao na haya makampuni".


"Pasaka hii inatufika tukiwa hoi na bando tu mengine yote Bye, Mhe Waziri ni kilio cha wapiga kura wetu lakini tusisahau sasa hivi dunia imebadilika kila jambo lipo kwenye simu na taarifa zote mitandaoni sasa kwa bando, hili tunahitaji huruma yako mzee mwenzangu embu simama sema na Watanzania kuhusu bando, nakuamini sana" ameongeza Steve Nyerere.


Mwanzoni mwa Machi, 2021 mkurugenzi mMkuu wa TCRA, James Kilaba aliahidi utekelezaji wa kanuni hizo za kukabiliana na malalamiko juu ya huduma ya vifurushi yaliyotokana na maoni 3, 278 yaliyotolewa na wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments