UZEMBE WA UKUSANYAJI WA MAPATO KWENYE MNADA WA MIFUGO WA PUGU WAMKERA WAZIRI NDAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akipitia rekodi za ukusanyaji na uingizaji wa mifugo mnadani katika mnada wa Pugu alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo leo Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mnada wa Upili Pugu Jijini Dar es Salaam Bw.Kerambo Samweli akitoa taarifa kuhusu uendeshaji wa mnada huo kwa Waziri wa mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki (hayupo pichani) mara baada ya Waziri kutembelea leo mnada huo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akisikiliza kero zinazowakumba wauzaji wa mifugo katika mnada wa mifugo Pugu Jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea mnada huo leo . Wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki mara baada ya kutembelea mnada wa Mifugo Pugu leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akizungumza jambo na Mkuu wa Mnada wa Upili Pugu Jijini Dar es Salaam Bw.Kerambo Samweli mara baada ya Waziri kutembelea leo mnada huo. Waziri wa mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mnada wa upili Pugu baada ya kutembelea mnada huo leo Jijini Dar es Salaam.

(Picha na Emmanuel Mbatilo)


NA EMMANUEL MBATILO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki ameelekeza Uongozi wa Mnada wa Mifugo Pugu Jijini Dar es Salaam kufikia Juni mwaka huu kuweza kukusanya mapato kufikia Bilioni 3 au zaidi.

Ameyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea mnada huo kuona maendeleo na changamoto zinazoukabili mnada huo.

Akizungumza katika ziara hiyo Mhe Ndaki amesema ukusanyaji mdogo wa mapato unaotokea katika mnada huo ni kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya viongozi wanaosimamia mnada huo.

"Nataka tarehe 30 Juni makusanyo yenu yawe Bilioni 3 au zaidi ndicho ninachotaka zaidi kwenye mnada huu, hayo ndio maelekezo yangu kwenu tufanyeni kazi kwa uadilifu tuacheni hizi kona kona". Amesema Mhe.Ndaki.

Pamoja na hayo Mhe.Ndaki amewaahidi watumiaji wa mnada huo kuukarabati ili kuweza kuondokana na kero zinazopatikana kwenye mnada huo hasa mifugo kupotea kutokana na kutokuwepo kwa uzio (ukuta) pamoja na ukosefu wa maji kwaajili ya mifugo.

"Mnada huu tutaukarabati miundombinu ya mnada huu kwasababu unatuingizia fedha nyingi, hatuwezi kukosa fedha ya kuweka tofali na ukuta kuzunguka mnada huu angalau tutaanza na hilo na mengine yatafuata ikiwemo maji kwaajili ya mifugo". Amesema

Aidha amewataka wafanyabiashara na wafugaji kuendelea kufanya kazi kwa uhuru kwani viongozi wa Serikali watendelea kuondoa changamoto ambazo wanakutana nazo wafanyabiashara ikiwemo changamoto ya tozo ambazo ni kero.

Kwa upande wake Mkuu wa Mnada huo Bw.Kerambo Samweli amesema mwaka jana waliweza kukusanya mapato na kupitiliza malengo lakini kwasasa wanaona haitawezekana kutokana na kupungua kwa uingiaji wa mifugo kwenye mnada huo kwa mwaka huu.

"Tulifanikiwa kukusanya zaidi ya malengo kwa mwaka 2018/2019 tulikusanya kwa 112% pia kwa mwaka wa 2019/2020 tumefanikiwa kukusanya kwa 88.8%". Amesema Bw.Kerambo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments