Hayati, Dkt. Magufuli Mwanamwema wa Afrika, Mwamba wa sekta ya Sanaa nchini


Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma
Kifo cha Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye alikuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si pigo tu kwa nchi, bali ni pigo katika tasnia ya Sanaa nchini. 


Akitoa hotuba yake wakati wa maombolezo ya Kitaifa ya Hayati, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwashukuru Watanzania kwa kuonesha umoja, mshikamano na upendo kwa kujitoa kwa moyo wakati wote tangu msiba utokee.


“Asanteni sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kumuaga kipenzi chetu, watu wametandaza nguo barabarani hii ni namna ya kuenzi utu wake, kazi zake alizofanya, uzalendo wake kwa taifa, maisha yake yote aliitanguliza Tanzania. Vizazi na vizazi watasimulia hadithi nzuri” alisema Rais Samia.
 

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa aliwashukuru wasanii kwa kuendelea kuimba nyimbo za maombolezo ambayo yatadumu kwa  siku 21 tangu kutokea kifo cha mpendwa wetu Hayati Dkt. Magufuli.


“Wasanii endeleeni kutoa faraja kwa kipindi chote kwa kutoa hisia zenu na kuwashirikisha Watanzania kufarijiana wakati wa kipindi chote cha kumuaga kipenzi chetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.


Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Awamu ya Kwanza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitambua umuhimu wa Sanaa na utamaduni katika taifa kwa kusema,  “Utamaduni ni kiini cha taifa lolote, nchi isiyo na utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu wasio na roho ambayo inayofanya taifa.”


Sekta ya Sanaa ni  nguvu laini (soft power) ya kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli zote za kijamii ambapo sekta hiyo inasimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. 


Ni dhahiri Dkt. Magufuli amekuwa Rais wa kwanza kuunda wizara yenye sekta ya sanaa inayojitegemea na kuwafanya wasanii watembee kifua mbele kwa kushiriki kazi mbalimbali za Serikali ikiwemo matamasha na dhifa za kitaifa.


Aidha, Hayati Dkt. Magufuli alijipambanua kwa kupenda kazi za Sanaa ambapo wakati wa uhai wake alipokuwa akitekeleza majukumu yake aliwatumia wasanii na kila mara alisikika akisema “Ni lazima wasanii wetu wanufaike na matunda ya kazi zao za Sanaa.” 


Tangu kutangazwa msiba wa Hayati Dkt. Magufuli Machi 17, 2021, tumeshudia wasanii mbalimbali wakiandaa na kuimba nyimbo za maombolezo zinazosadifu utendaji kazi wake ambazo wanaendelea kuziwasilisha kwa jamii kwa umahiri mkubwa kwa kuwapa familia na Watanzania faraja.


Enzi za uhai wake akiwa kiongozi Mkuu wa nchi, katika moja ya hotuba zake Dkt. Magufuli akihitimisha Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma, Juni 16, 2020 alisema Sanaa ni sekta ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.   


“Sekta nyingine, ambayo haijasemwa sana lakini kwa sasa ina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu ni sanaa na utamaduni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2018, shughuli za Sanaa na Burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo ilikua kwa asilimia 13.7 na mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia 11.2, hongereni sana wasanii wetu mbalimbali, hususan wa Bongo Fleva na Filamu. Kazi zenu sio tu zinaburudisha na kuchangia ukuaji uchumi, lakini pia zinaitangaza nchi yetu kimataifa”, Hayati Dkt. Magufuli.


Katika maombolezo ya msiba huu, wasanii kupitia tungo zao wameonesha jinsi walivyoguswa wakisema Dkt. Magufuli amewaachia Watanzania majonzi, simanzi kwenye mioyo yao.
Moja ya wimbo waliotunga wasanii umebainisha kuwa kazi aliyoitiwa duniani Dkt. Magufuli ameimaliza, ametumika kikamilifu utumishi wake hautasahaulika nchini, nenda salama tutakukumbuka daima buriani Mwanamageuzi mahiri.


Wakati wa maombolezo ya kitaifa yaliyofanyika Machi 22, 2021 Wasanii “Tanzania all-stars”  waliimba wimbo maalum usemao “Tusihuzunike bado tumaini lipo”, tutakukumbuka daima maana tulikupenda sana, pumzika kwa amani.”


Ujumbe wa wasanii hao unaonesha umahiri wa jinsi Dkt. Magufuli alivyoongoza nchi na kuheshimu kazi yake ya kishujaa, kijasiri na uhodari katika kufanya mapinduzi ya kweli katika sekta mbalimbali ikiwemo sanaa na kusema Watanzania wataikumbuka kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu.’ 


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni  Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hasaan Abbasi amesema “Katika uhai wake kama kuna kitu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikipigania na kukipangia kukipigania zaidi kikue zaidi ni sekta ya sanaa.


Katika kampeni zake wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, neno wasanii lilikuwa kinywani mwake sana, kiasi cha kuambatana nao kwenye kampeni zake. Taswira hiyo ilianza kuonekana tangu mwaka 2015 ambapo amekuwa Rais wa kwanza kuunda wizara yenye sekta ya sanaa kama sekta inayojitegemea.


“Leo hatuko naye mtu huyu Dkt. John Pombe Magufuli, bingwa katika kuipigania sekta ya sanaa, anapaswa kuimbiwa, nyimbo za maombolezo, nyimbo za kumwombea pumziko la amani na la milele. Hivyo Machi 25 kuanzia saa 10 kamili jioni hadi saa moja katika uwanja wa Magufuli hapa Chato tumewapa nafasi wasanii wote watakaoweza kufika Chato na waliokwishafika Chato kumuimbia Magufuli kwa nyimbo mbalimbali za maombolezo walizozitunga mmoja mmoja na kama makundi,” alisema Dkt. Hasaan Abbasi 


Kwa kutambua na kuthamini kazi ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, baadhi ya wasanii wameshiriki kuimba kwa pamoja wimbo maalum wa maombolezo chini ya usimamizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).


Wasanii hao ni pamoja na Nandy, Marioo, Dogo Janja, Young Lunya, GoodLuck Gozbeth, Christina Shusho, Majid, JayMelody, Khadija Kopa, Mzee Yusuph, Mrisho Mpoto, Jesca Mshama, Linah, Hamadai, Whozu, Stamina, Merissa, Meja Kunta, Mzee Kalala na Ndelah.
Mwisho.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments