BURUNDI YAIOMBA TANZANIA KUISEMEA KIMATAIFA


Burundi imeiomba Tanzania kuendelea kuisemea nchi hiyo katika majukwaa ya Kimataifa ili iweze kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Jumuiya ya Ulaya jambo linalozorotesha  maendeleo ya kiuchumi kwa nchi hiyo.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaendeleo wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi unaofanyika kwa ngazi ya wataalam mjini Kigoma tarehe 3 na 4 Machi 2021.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge amesema Tanzania itaendelea kuisemea Burundi katika majukwaa ya Kimataifa ili Burundi iondolewe vikwazo vyote vya kiuchumi ilivyowekewa ili kuipa nafasi nchi hiyo kuendelea na jitihada za kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Pamoja na hilo Balozi Ibuge ameihakikishia Burundi kuwa, Tanzania itaendelea na jitihada zake za kuisadia nchi hiyo kuingia katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili iweze kuungana na nchi za ukanda huo katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.

“Tanzania na Burundi zimeendelea kushirikiana kwenye Nyanja za Kimataifa na Kikanda kupitia Jumuiya za EAC, ICGLR, AU na Umoja wa Mataifa (UN). Ni kupitia ushirikiano huu, Tanzania itaendelea kuisemea Burundi katika majukwaa ya kimataifa ili iondolewe vikwazo vyote vya kiuchumi ilivyowekewa. Na kwa mara nyingine na uhakikishia ujumbe wa Burundi kwamba Tanzania itaendelea kuunga mkono ombi la nchi hiyo la kuwa mwanachama wa SADC” alisema Balozi Ibuge.

Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge alieleza kwamba Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ni fursa nzuri ya kujadili masuala mbalimbali yenye manufaa kwa nchi zote mbili na kuwataka wajumbe wa mkutano huo kujipanga kutekeleza kikamilifu yale yote yatakayokubalika katika mkutano huo.

Mkutano huu umeanza kwa ngazi ya wataalam na utamalizika kwa ngazi ya Mawaziri tarehe 5 Machi 2021 ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa AFrika Mashariki ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post