TANZANIA NA BURUNDI ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza kama Mwenyekiti wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi uliofanyika kwa ngazi ya Mawaziri mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021. Wengine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje Burundi na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo Mhe. Balozi Albert Shingiro ( wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (wa pili kutoka kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba (kushoto). Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Wataalam ulifanyika tarehe 3 na 4 Machi 2021.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Balozi Albert Shingiro akizungumza wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi ulifanyika kwa ngazi ya mawaziri mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021

***
Tanzania na Burundi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya nchi hizo ulimalizika mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021.

Makubaliano yaliyofikiwa yamejikita kwenye maeneo kuimarisha sekta za siasa na mahusiano ya kidiplomasia, ulinzi na usalama, maendeleo ya miundombinu, ushirikiano katika sekta ya uchumi na kijamii.

Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wa watu wake kupitia jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi nyingine ikiwemo Burundi.

Ameongeza kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kujenga uchumi na kuinua maisha ya watanzania. Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeendelea kuwekeza na kuboresha sekta mbalimbali pamoja na kujenga miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na ujenzi wa Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219.

Alisisitiza mbali na jitihada hizo, upo umuhimu mkubwa wa Tanzania kushirikiana na nchi nyingine ikiwemo Burundi ili mafanikio haya yawe na tija zaidi kwa wananchi. “Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Magufuli imeendelea kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ili kukuza uchumi wa wananchi wake. itihada hizi haziwezi kufanikiwa kama Tanzania haitashirikiana na nchi nyingine na kama Tanzania haitawahimiza wananchi wake kuvuka mipaka na kufanya biashara na wenzao wan chi nyingine. Ni kwa msingi huo Mkutano huu wa Tume ya Pamoja ya kudumu una umuhimu mkubwa kwa nchi zetu mbili hususan kuingia makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali” alisisitiza.

Kadhalika alisema kuwa maeneo ya ushirikiano yaliyokubalika kwenye mkutano huo ni sehemu tu ya maeneo mengi muhimu ambayo Tanzania na Burundi zitaendelea kuyaibua kadri ushirikiano huo unavyoendelea.

“Kuna maeneo mengi sana ambayo nchi zetu zinaweza kushirikiana, ni dhahiri mpaka sasa hatujaweza kuzitumia fursa zote zilizopo. Tumeanza na sekta za ulinzi na usalama; biashara na uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi inayounganisha nchi hizi pamoja na masuala ya kijamii na tutaendelea kuvumbua maeneo mengine mapya ya ushirikiano kadri tunavyoimarisha ushirikiano huu” alisema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi alitumia fursa hiyo kuzihimiza sekta zinazohusika na usimamizi wa miradi ya kikanda ya miundombinu inayotekelezwa na Serikali za Tanzania na Burundi chini ya uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiwemo mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (260km) na Barabara ya Rumonge-Gitaza (45km) na ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Manyovu/Mugina kutekeleza kikamilifu ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Tanzania na Burundi.

Pia alitoa rai kwa watendaji wa Tanzania na Burundi kusimamia kikamilifu utelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ili mikutano ya tume iwe yenye tija.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu, Mhe. Balozi Albert Shingiro alisema nchi yake imedhamiria kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa na kutaja mkutano wa sita kama mwanzo mzuri wa kuendeleza ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Burundi.

Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi umehitimishwa kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano kwenye maeneo matano ambayo ni Ushirikiano wa Kidiplomasia; Ulinzi na Usalama; Uendelezaji Miundombinu ya Usafirishaji; Elimu na Utamaduni na Biashara na Uwekezaji. Kadhalika Mkutano huo umeshuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chemba za Biashara za Tanzania na Burundi ukiwa na lengo la kuimarisha biashara baina ya nchi hizi mbili.

Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ambao umefanyika mjini Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021 umehudhuriwa na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na viongozi wengine waandamizi kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Burundi.
Balozi Ibuge nae akizungumza wakati wa mkutano sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi uliofanyika kwa ngazi ya Mawaziri
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akiwakaribisha Mkoani Kigoma Viongozi na Wajumbe walioshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ulifanyika kwa ngazi ya mawaziri
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kwenye maeneo kadhaa yaliyojadiliwa na kukubalika wakati wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tannzania na Burundi
Mawaziri wakibadilishana Hati hizo baada ya kusaini
Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCA), Bw. Paul Koyi kwa pamoja na Kaimu Rais wa Chama cha Wafanyabiasha cha Burundi, Bw. Tharcisse Havyarimana (kushoto) wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kwenya masuala ya Biashara na Uwekezaji.
Sehemu ya Mawaziri na Makatibu wakuu na Viongozi wengine kutoka Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi uliofanyika kwa ngazi ya mawaziri tarehe 5 Machi 2021.
Sehemu nyingine ya Makatibu Wakuu wakifuatilia matukio mbalimbali ya mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi
Ujumbe wa Tanzania wakati wa mkutano
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Buhohela akitoa ratiba ya masuala mbalimbali yanayoendelea wakati wa mkutano wa sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi
Ujumbe wa Burundi
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Frank Mwega (kulia) akiwa na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi
Mhe. Prof. Kabudi akimpatia Mhe. Balozi Shingiro zawadi ya picha ya michoro maarufu ya Tingatinga zinazopatikana hapa nchini
Mhe. Prof. Kabudi akimbidhi Mhe. Balozi Shingiro Kamusi ya Kiswahili ili kumwezesha kuendelea kuongeza msamiati wa Kiswahili ikiwa ni Lugha iliyokubalika kufundishwa nchini Burundi.
Mhe. Balozi Shingiro akimkabidhi Mhe. Prof. Kabudi zawadi ya kikapu kinachotambulisha utamaduni wa Burundi
Makatibu Wakuu nao wakipeana zawadi ambapo Balozi Ibuge anaonekana akimkabidhi Mhe. Ntirampeba zawazi ya Kamusi ya Kiswahili
Mhe. Ntirampeba nae akikabidhi zawadi kwa Balozi Ibuge
Viongozi wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja
Meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jillyy Maleko ( wa tatu kushoto waliosimama)
Meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya maandalizi ya Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja naMhe. Balozi Shingiro wakifurahia kikundi cha ngoma maarufu kama Mapigo Tisa cha mkoani Kigoma kilichotumbuiza wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments