WIVU WA MAPENZI, USHIRIKINA BADO CHANZO CHA MATUKIO YA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO HALMASHAURI YA SHINYANGA


Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba
**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Imeelezwa kuwa licha ya matukio ya ukatili kupungua katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga lakini bado kuna changamoto ya imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi na ugomvi wa kifamilia kuhusu urithi wa mashamba vinachangia kuendelea kutokea kwa matukio ya ukatili kwenye baadhi ya maeneo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba wakati akizungumza na Malunde 1 blog ambapo amesema matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada kubwa zinazofaywa na halmashauri hiyo kwa kushirikiana na jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Women Fund Tanzania (WFT).

"Licha ya matukio ya ukatili kupungua kwa kiasi kikubwa katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga lakini bado kuna changamoto ya imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi na wakati mwingine kuna matukio yanahusisha ugomvi wa kifamilia kuhusu mashamba.

“Matukio mengi yanayohusisha akina mama mengi yanahusisha wivu wa kimapenzi au imani za kishirikina na kwa upande wa watoto ni suala linahusu zaidi malezi ambapo wazazi wanawapa watoto uhuru wa kuzurura hovyo matokeo yake wanapata ujauzito",ameongeza Mahiba.

Ameeleza kuwa kuna baadhi ya familia zinamuona mtoto wa kike kama kitega uchumi ambapo kuna watoto ambao wanaozeshwa wakiwa wadogo, mzazi anawaza atapata ng’ombe wangapi akieleza kuwa pia bado kuna tamaduni mila na desturi kandamizi ambapo baadhi ya watu wanaamini kuwa mtoto wa kike ni wa kuolewa tu.

"Tunaendelea kuelimisha jamii yetu waweze kuwaona watoto wa kike sawa sawa na watoto wa kiume hivyo wanastahili kupata elimu. Tayari tumetoa mafunzo kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ngazi ya kata na vijiji na halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa ukatili wa kijinsia",ameeleza .

Aidha amesema wanaendelea kuielimisha jamii kuwa hakuna urithi mzuri kwa mtoto kama elimu hivyo wawaache watoto wasome badala kukatisha ndoto zao.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Pandagichiza akiwemo Jeremiah Seleli licha ya kukemea mila na desturi Kandamizi na imani za kishirikina wameomba serikali kuwachukulia hatua baadhi ya waganga wa kienyeji wanaooa watoto na watu wenye pesa ambao fedha zao zinawafanya kuwa na kiburi cha kufanya jambo lolote wanalotaka matokeo yake wanaolewa kwa siri kubwa.

Daniel Charles na Monica Nyanda wameomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya viongozi wa ngazi ya kata na kijiji wanaogeuza kesi za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake kuwa chanzo cha kipato hali ambayo inachangia matukio ya ukatili kuendelea kutokea.

Naye Nyamizi Ndaki ameiomba jamii kuacha imani za kishirikiana kwa kutoendekeza waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakiwadanganya na kujikita wakifanya ukatili kama vile kubaka na kuua watu wasio na hatia.

Mara kwa mara Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amekuwa akihubiri kuhusu wajibu wa kila mtu katika jamii kushiriki kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto akisisitiza kuwa Ukatili wa kijinsia ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine.

Mboneko amekuwa akihamasisha kuwa pindi matukio ya ukatili ikiwemo ubakaji, mimba na ndoa za utotoni yanapotokea wananchi watoe taarifa kwenye vyombo vinavyohusika ili hatua zichukuliwe haraka kwani serikali inataka watu wote wawe salama.

Wito mwingine wa Mkuu huyo wa wilaya ni viongozi wa serikali kuanzia wa serikali za mitaa kusimamia ipasavyo haki za binadamu kwa kutoyafumbia macho matukio ya ukatili bali wachukue hatua haraka.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Desemba 2,2020 yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba anasema hivi sasa kuna mwamko mkubwa wa jamii kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia akitolea mfano kuwa katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2020 kumeripotiwa matukio 231 ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikilinganishwa na kipindi cha Mwezi Juni hadi Agosti mwaka 2019 ambapo kulikuwa na matukio 151 ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Tunashukuru wananchi wameanza kuziamini ofisi za madawati ya jinsia takribani matano tuliyonayo katika mkoa wa Shinyanga ambapo wamekuwa wakitoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia. Lakini pia tunazishukuru taasisi na mashirika tunayoshirikiana nayo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia”,alisema Kamanda Magiligimba.

“Naomba pia wazazi na walezi waache kumaliza kesi za matukio ya ukatili wa kijinsia kifamilia. Mzazi usikae na kusuluhisha kesi ya mtoto kufanyiwa ukatili,toa taarifa ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria ili kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia”,aliongeza.

Aidha Kamanda huyo anazitaka familia kuacha kuficha matukio ya ukatili wa kijinsia na kulipana fidia watoto wakifanyiwa ukatili ili kumaliza kesi na kuhakikisha wanatoa ushahidi kuhusu matukio hayo sambamba na kuepuka kutoa ushahidi wa uongo hali ambayo inakwamisha kesi za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post