WAZIRI UMMY ATOA RAI KWA WACHIMBAJI WA MCHANGA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu  akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Bagamoyo katika ziara yake hii leo Mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Bagamoyo katika ziara yake hii leo Mkoani Pwani. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Zainab Kawawa na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Mhe. Mwarami Mkenge.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Bw. Hassan Wembe mmiliki wa machimbo ya mchanga katika Kitongoji cha Kitopeni Kata ya Kiromo Wilayani Bagamoyo leo Februari 17, 2021 na kumuelekeza kutekeleza mpango wa kurejesha ardhi mara baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika. Waziri Ummy Mwalimu yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu (3) yenye lengo la kukagua shughuli za utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira


Miti aina ya Mikoko ikiwa imeoteshwa ikiwa ni sehemu ya kurejesha uoto wa asili na bioanuai katika Kitongoji cha Kondo na Mlingotini Wilayani Bagamoyo.

Sehemu ya machimbo ya Mchanga kama inavyooneka kukiwa na uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na uchimbaji holela wa mchanga na ukataji wa miti.

 ***

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu amesema ipo haja ya kuweka tozo maalumu ya kurejesha hali ya mazingira kutokana na na athari za uchimbaji wa mchanga kama ilivyo kwenye migodi mikubwa katika maeneo ya Bagamoyo Mkoani Pwani.

Akikagua maeneo ya uchimbaji wa mchanga katika eneo kitongoji cha Kitopeni, Kata ya Kiromo Wilayani Bagamoyo, Waziri Ummy amesema suala la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ni jukumu letu sote na kusisitiza kuwa ni wajibu wa wachimbaji kuwa na mpango wa kurejesha mazingira katika hali yake ya awali baada ya kumaliza shughuli za uchimbaji.

“Tunataka kuona mwekezaji anatekeleza mpango wa kurejesha mazingira katika hali yake ya awali mara baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika” Ummy alisisitiza.

Amesema uchimbaji wa mchanga uendane na hifadhi ya mazingira na kusisitiza kuwa azma ya Serikali ni kulinda afya za watu wake na mazingira yanayowazunguka hivyo wajibu wa kurejesha ardhi kama ilivyokuwa awali ni wajibu wa mwekezaji.

Waziri Ummy pia ameitaka jamii ya Pwani kuhakikisha wanatunza mikoko kwa manufaa ya mazingira ya bahari na bioanuai kwa kubuni chanzo mbadala cha mapato na kutolea mfano ulimaji wa kilimo cha mwani badala ya ukataji wa mikoko kwa matumizi ya kuni na mkaa na ameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kupanda ekari 22 za mikoko kupitia mradi wa TASAF.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bi. Zainab Kawawa amesema biashara ya uchimbaji mchanga ni chanzo kikubwa cha mapato katika Halmashauri yao na kusisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ili kuwa shughuli za uchimbaji mchanga ziwe endelevu.

“Ipo haja ya kuainisha maeneo ya kuchimba mchanga na si kila eneo ni sahihi kwa uchimbaji” Bi. Kawawa alisisitiza.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara ya kukagua shughuli za utunzaji na uhifadhi wa mazingira Waziri Ummy Mwalimu hii leo ametembelea Kitongoji cha Kitopeni, Kata ya Kiromo, Vitongoji vya Kondo na Mlingotini.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post