WAFANYABIASHARA WAMETAKIWA KUSAJILI BIDHAA NA MAJENGO YA VYAKULA KUENDANA NA MATAKWA YA SHERIA

 

Afisa udhibiti ubora wa TBS Bw. Anderson Msumanje akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa wa TPRI Dkt. Ephrahim Njau alipotembelea banda la TBS. Afisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi Neema Mtemvu akitoa elimu kwa wadau mbalimbali waliotembelea katika banda la TBS kwenye maonesho ya nne ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayoendelea mkoani Arusha. 

 Katika maonesho haya wananchi wamepata fursa ya kupata elimu ya Viwango na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS. Mtemvu alitoa wito kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwenda TBS kusajili majengo ya vyakula na vipodozi na kuthibitisha bidhaa ili waweze kupata masoko ya uhakika .

Wananchi wakipata fursa ya kupata elimu ya Viwango na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS.


Na Mwandishi Wetu, Arusha

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiasha kujitokeza kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za walaji.

Wito huo umetolewa na afisa uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu kwenye Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyoanza Ferbruari 7, mwaka huu hadi 13 jijini Arusha yakiwa yameandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Shirika hilo linashiriki maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu ya viwango kwa wananchi, wajasiriamali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali na msisitizo wao mkubwa ni ujenzi wa Tanzania ya viwanda na kukua kiuchumi.

"Tunatoa wito kwa wanaofika kwenye maonesho haya kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019," alisema Mtemvu.

Sheria hiyo ilirudisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA).

"Kwa hiyo usajili wa bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria ili kuwawezesha kufanyabiashara zao urahisi," alisema Mtemvu wakati akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa wananchi waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonesho hayo.

Alisema usajili majengo ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza bidhaa na kwamba wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazoenda kuhifadhiwa humo.

Kwa upande wa usajili wa bidhaa, Mtemvu alisema eneo linalohusika ni bidhaa za chakula na vipodozi .

Alisema usajili wa vipodozi unalenga kuhakikisha vipodozi vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania haviingizwi nchini kutokana na kuwa na viambata sumu.

Wakati huo huo, Mtemvu ametoa wito kwa wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kuthibitisha ubora wa bidhaa zao TBS bure, kwani gharama hizo zinalipwa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha kufanyabiashara.

Alisema wanachotakiwa kuwa nacho ni barua ya utambulisho kutoka SIDO na baada ya hapo wakifika TBS mchakato unaanza mara moja. Alisema wamefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye maonesho hayo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post