SOMO LA HISTORIA YA TANZANIA KUANZA KUFUNDISHWA RASMI JULAI 2021 KWA LAZIMA...SHULE YA MSINGI HADI KIDATO CHA SITA

Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

SERIKALI Imesema Somo la Historia ya Tanzania litaanza kutumika kwa lazima  kwa wanafunzi wote kuanzia mwezi Julai Mwaka huu lengo likiwa kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na uzalendo na kuwatambua mashujaa wote wa Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Februari 12,2021 Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Profesa Ndalichako amesema katika kuzingatia maelekezo ya Rais  wa Tanzania Dkt.John Magufuli, Somo hilo la Historia lisomwe na wanafunzi wote,na mihtasari imeandaliwa kusoma somo hilo la Historia kuanzia Elimu ya awali.

Aidha amesema Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuchapisha vitabu na vitakamilika mwezi Machi mwaka huu ambapo Somo litaanza kufundishwa Mwezi Julai ,2021.

Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako amebainisha kwamba Wizara Elimu Sayansi na Teknolojia inashirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo katika uandaji wa mihtasari.

"Nasisitiza watunzi wa vitabu lazima wahakikishe wanaandika kwa ufasaha hivyo Sisi kama Wizara tunashirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo katika kuandika," amesema Profesa Ndalichako.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dkt Leonard Akwilapo amesema Somo la Historia ya Tanzania litafundishwa kwa lugha ya Kiswahili kuanzia darasa la Kwanza  hadi kidato cha Sita. 

Ikumbukwe kuwa Rais wa Tanzania  Dkt John Magufuli Wakati akiapisha mawaziri na Manaibu Mawaziri Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma mnamo tarehe 9 Desemba 2020 aliagiza Somo la Historia ya Tanzania loanze kufundishwa mashuleni ili kujenga uzalendo  na kuwafanya wanafunzi kujua walikotoka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post