TCRA YAIPUNGUZIA ADHABU WASAFI TV HADI FEBRUARI 28 | MALUNDE 1 BLOG

Thursday, February 4, 2021

TCRA YAIPUNGUZIA ADHABU WASAFI TV HADI FEBRUARI 28

  Malunde       Thursday, February 4, 2021


Na Herieth Makwetta - Mwananchi
 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeipunguzia adhabu televisheni ya Wasafi TV kutoka kifungo cha miezi sita na kuiruhusu kuendelea kurusha matangazo yake kuanzia Februari 28, 2021.

Januari 5, 2021 TCRA ilitoa uamuzi wa kuifungia televisheni hiyo kwa kipindi cha miezi sita kutokana na kukiuka kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na Posta.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 4, 2021 na mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba imetaja masharti matatu kwa televisheni hiyo ikiwemo kuendelea kutumikia kifungo hicho mpaka tarehe tajwa.

“Wasafi TV itaendelea kutumikia adhabu hiyo mpaka Februari 28, 2021 pia inaelekezwa kuzingatia masharti ya leseni ya kutoa huduma za maudhui ya kulipia kwa njia ya televisheni na iwapo itashindwa, itakataa au kukaidi uamuzi huu hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa dhidi ya yake,” ameeleza.

Kilaba amesema kufuatia uamuzi wa kuifungia, Januari 21, 2021 Wasafi iliwasilisha maombi TCRA na vielelezo zaidi ikiomba kupitia upya uamuzi wake na Januari 28, 2021 ilifika tena kwa ajili ya kusikilizwa maombi hayo.

Amesema Wasafi iliwasilisha ushahidi mpya kuonyesha kuwa endapo ushahidi huo ungewasilishwa awali wakati wa usikilizwaji, TCRA isingetoa adhabu ya kuifungia miezi sita.

Amebainisha kuwa televisheni hiyo ilikiri kurusha matangazo mubashara kinyume na masharti ya leseni yao, na iliomba TCRA kupitia upya uamuzi wake na kuwapunguza adhabu.

“Baada ya kusikiliza wasilisho la Wasafi, TCRA imetafakari upya uamuzi wake wa Januari 5, 2021 kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na Wasafi baada ya kosa kutendeka na hivyo basi TCRA imepunguza adhabu hiyo,” amesema Kilaba.

CHANZO - MWANANCHI


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post