RAIS MAGUFULI ATAKA WATANZANIA WAFANYE MAOMBI, WAFUNGE SIKU 3 VITA DHIDI YA CORONA....ASISITIZA 'TUSITISHANE NA KUOGOPESHANA'


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa amekaa kwa majonzi wakati mwili wa Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ulipowasili kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19,2021 ambako ataongoza shughuli za kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kuaga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa la Tanzania dhidi ya Ugonjwa wa Corona na kusisitiza kuwa hatatangaza Lockdown.

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akiongoza waombozaji kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19,2021.

"Tusitishane na kuogopeshana Mungu yupo, Mungu ndiyo muweza wa yote, Tuendelee kusimama na Mungu, tulishiinda Corona mwaka jana. Naomba Tusimame na Mungu. 

"Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, magonjwa ya vifua, magonjwa ya kupumua na kadhalika yatakuwepo na hayakuanzia hapa, Zipo Nchi ambazo zimepoteza watu wake wengi. Sisi Tanzania Mungu ametusaidia sana mwaka uliopita, tuendelee kuchukua tahadhari huku tukimuomba Mungu. Mungu Hashindwi",amesema Rais Magufuli.

"Naomba tusitegemee nguvu za ubinadamu, bali tumtegemee Mungu. Narudia ndugu zangu tujue Mungu yupo. Mungu ndiyo muweza wa yote. Nashukuru viongozi wa dini mmeendelea kulihubiri hilo. Tuendelee ndugu zangu kusimama na Mungu. Tulishinda mwaka jana, inawezakana hili ni jaribu jingine, nalo tukisimama na Mungu tutashinda", - Rais Magufuli.

Tusitishane na kuogopeshana, tutashindwa kufika. Inawezekana kuna mahali tumemkosea Mungu. Inawezeakana kuna mahali tunapata jaribu kama wana wa Israel walivyokuwa wanaenda Kaanani. Tusimame na Mungu ndugu zangu Watanzania. Kufa tutakufa tu,unaweza kufa kwa malaria,ukafa kwa Kansa,ukafa kwa magonjwa mengine kwa sababu kufa kupo lakini Kamwe tusimuache Mungu. Huo ndiyo wito wangu", amesema Rais Magufuli.

"Tusimame na Mungu ndugu zetu Waislamu walitangaza muda wao wa kuomba na niliambiwa na Mufti,niwaombe tena Watanzania kama kuna mahali tumetereka tuendelee kumuomba Mungu. Tuanze leo kwa ndugu zetu Waislamu,kesho Jumamosi kwa ndugu zetu Wasabato wanaosali Jumamosi na Jumapili kwa ndugu zetu Wakristo kwa kumuomba kufunga kwa siku tatu. Mimi nina uhakika tutashinda. Nataka niwape nguvu hiyo ndugu zangu Watanzania",ameongeza Rais Magufuli.

"Naomba  Viongozi wa dini muendelee kusisitiza maombi. Tulishinda mwaka jana, tutashinda mwaka huu, tutashinda miaka yote  kwa sababu kamwe Mungu hajaweza kuliacha taifa hili.Tumeshinda mwaka jana na tukaingia kwenye uchumi wa kati na Corona ipo,uchumi ukaendelea kupanda na Corona ipo,miradi ikaendelea kutekelezwa wala hatukuweka Lockdown hata sasa hatutaweka Lockdown kwa sababu tunajua Mungu yupo siku zote. Taifa hili lipo mikononi mwa Mungu",amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amesitikitishwa na watu wanaozusha taarifa za uongo kwamba Waziri wa Fedha,  Dk. Philip Mpango amefariki dunia huku akisoma SMS aliyotumiwa na Dk. Mpango kuhusu hali anayoendelea nayo.

"Imefikia mahali sasa tunatishana sana.Leo asubuhi nilitumiwa Meseji na Waziri wa Fedha Dk. Mpango ambaye amelazwa Dodoma na ninaomba niiosome hapa kwa faida ya wale waliokuwa wana Twitt kwamba amekufa",amesema.

Rais Magufuli amesema katika SMS hiyo, Dkt. Mpango amemueleza Rais Magufuli kuwa kwa Neema ya Mungu anaendelea vizuri, anakula vizuri na anaendelea kufanya mazoezi ya kifua na kutembea na kwamba wale waliomzushia mtandaoni kuwa amefariki dunia amewaombea kwa Yesu wakati wa Sala ya Jioni jana.

Akimzungumzia Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu na kuzikwa jana Mtamwe wilayani Wete kisiwani Pemba, Zanzibar, Rais Magufuli amesema baada ya kufanya mazungumzo na aliyekuwa  alibaini kuwa Maalim Seif alikuwa ni kiongozi wa tofauti.

“Maalim Seif alikuwa ni kiongozi wa tofauti sana mwaka 2015 nilipokuwa rais baada ya uchaguzi wa Zanzibar kufanyika ule wa marudio, Maalim Seif aliniandikia barua akiniomba kuja kuniona nilisita kidogo kwamba kwa nini anataka kuja kuniona na wakati hata kwenye uchaguzi hakushiriki, Maalim Seif akaandika tena barua ya pili na baadaye akaandika barua ya tatu”.

“Kila nilipokuwa najaribu kupata ushauri kutoka Zanzibar nilikuwa naambiwa nisubiri nimuache lakini baadaye nikaamua ngoja nimuone Maalim Seif. Alipokuja Ikulu Dar es salaam nilipoanza kuzungumza naye nilimuona mtu tofauti sana na jinsi picha ilivyokuwa imejengeka kwa sababu mazungumzo yetu yalikuwa mazuri sana”,ameeleza.

Rais Magufuli amesema Maalim Seif alimueleza kuwa hakushiriki kwenye uchaguzi wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi, 2016 baada ya ule wa Oktoba 25, 2015 kufutwa akisisitiza kuwa licha ya jambo hilo kutokea lakini Zanzibar itakuwa salama na kwamba hatohamasisha fujo.

Akiendelea kumnukuu Maalim Seif, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema, “...Pili lakini nataka kukuhakikishia Zanzibar itakuwa salama sitahamasisha fujo yoyote na miaka yote mitano aliyechaguliwa ataendelea vizuri kutawala kauli hiyo niliiona mpaka baada ya miaka mitano alieleza yeye anapenda amani na angependa Zanzibar na Watanzania wote wakae kwa amani kauli hiyo niliithibitisha kwa vitendo ulipotokea uchaguzi mwingine Maalim Seif bado alishiriki katika Serikali ya Muungano, Serikali ya umoja.”

“Alikuwa ni mtu mcheshi na siku zote katika ziara yake hata kule Chato alikuwa akihubiri umoja wa Wanzanzibar umoja wa Watanzania kitu ambacho amemaliza nacho, Maalim Seif amemaliza salama na dhamira yake ya kuijenga amani na Wazanzibari na Watanzania kwa pamoja”,amesema.

“Natoa pole kwa Watanzania wote kwa vifo vyote viwili, cha Maalim Seif pamoja na cha Balozi Kijazi, Jana nilimtuma Makamu wa Rais na Dkt. Bashiru waniwakilishe kwenye mazishi ya Maalim Seif". Kijazi ameondoka hapa duniani kama Shujaa, Maalim Seif kaondoka hapa duniani kama shujaa".

“Balozi Kijazi na Maalim Seif wametangulia zamu yetu sisi bado, Watanzania katika matatizo yoyote yanapotokea yatufanye tuwe wamoja, hofu ni mbaya, ukiona kitu hauwezi kukitatua wewe, mwambie Mungu ndiye muweza, tumekuwa tunatishana sana, tusitishane", amesema Rais Magufuli

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments